WARSHAWA,POLAND

SHIRIKA la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limesema Poland iliwarejesha kinyume cha sheria wahamiaji waliokwama kwenye mpaka wake na Belarus.

Taarifa hiyo ilichapishwa kupitia uchunguzi uliofanywa wa picha za satelaiti na picha nyengine pamoja na video za Amnesty International.

Shirika hilo limesema kwa kutumia picha za satelaiti za kuanzia Agosti 18, lilifanikiwa kugundua kurejeshwa kwa wahamiaji hao waliokuwa wamekwama kwenye mpaka huo kwa wiki kadhaa.

Eve Geddie, mkurugenzi wa Amnesty International barani Ulaya, alisema kitendo cha wahamiaji hao waliokuwa wakijaribu kuomba hifadhi kulazimishwa kuondoka bila kupatiwa mahitaji muhimu ni kinyume cha sheria za Ulaya na kimataifa.

Wahamiaji hao hawana uwezo wa kupata maji, chakula au dawa.

Poland, Lithuania na Latvia zimeripoti kuongezeka kwa kasi wahamiaji kutoka nchi kama vile Afghanistan na Iraq, wanaojaribu kuingia kwenye nchi hizo kupitia mipaka ya Belarus.