NAIROBI, KENYA
MAOFISA sita wa polisi nchini Kenya wamefunguliwa mashitaka ya mauaji kutokana na vifo vya ndugu wawili wakati wakiwa kizuizini kwa tuhuma za kukiuka amri ya kutotoka nje kwa Covid-19.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mauaji ya Benson Njiru mwenye umri wa miaka 22 na ndugu yake Emmanuel Mutura Ndigwa mwenye umri wa miaka 19 yalipelekea maandamano makali, kulalamikia ukatili wa polisi.
Miongoni mwa maofisa sita waliofunguliwa mashitaka, wawili kati yao ni wanawake na wote walikanusha mashitaka mahakamani huku wakiamuriwa wabaki rumande hadi Septemba 22 shauri la dhamana litakaposikilizwa.
Ndugu hao wanaodaiwa kuuwawa walionekana mara ya mwisho Agosti mosi walipokamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwa nje wakati wa curfew baada ya saa nne za usiku.
Miili yao ilipatikana siku mbili baadaye na wanafamilia kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha mji wa Embu kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu.
Polisi walidai kwamba wawili hao waliruka kutoka kwenye gari lao, madai ambayo yalikanushwa vikali na wanafamilia pamoja na wanaharakati.