NA MADINA ISSA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, limesema linaendelea na msako wa kumtafuta mtu aliyefanya tukio la uvunjivu wa haki za binaadamu la kuwacharaza mapanga watu wawili akiwemo mama na mwana maeneo ya Fuoni nyumba Moja.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Ofisini kwake Mwembemadema, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Awadh Juma Haji, alisema, bado jeshi hilo, linaendelea kumsaka na linahakikisha linamtia mkononi mtuhumiwa huyo.

Alisema tukio hilo la kusikitisha lilitokea Agosti 31 majira ya saa 8 mchana huko Fuoni Nyumba moja ambapo mama aliyejukana kwa jina la Raya Khamis Mgeni miaka 46 na mwanawe Thumaisia Makame Khatib, mwenye umri wa mienzi 11, wakaazi wa Fuoni Nyumba Moja ambao walijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga maeneo ya kichwa na kuumia vibaya.

Alisema, mara baada ya tukio hilo, majeruhi hao walifikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja, ambapo mtoto akiwa anaendelea na matibabu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano juu ya tukio hilo, ili kuweza kumkamata mtuhumiwa wa tukio hilo ambaye aliingia ndani chumbani na kukuta mtoto akinyonyeshwa na kuanza kuwashambulia akiwaacha wana majeraha makubwa ya kuvuja damu.

Sambamba na hayo, alisema kuwa tukio hilo, ni sehemu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu jambo alilolifanya ambalo linastahiki kulaaniwa kwani ni la kinyama ndio maana wameanzisha msako, ili kumtia mikoni na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, mama huyo, ambae kwa sasa amelazwa katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja, alisema, mtu huyo aliyefanya tukio hilo, anaonekanwa ametumwa na mtu kwani haonekanwi na dalili ya wizi.

Alisema, alikuwa akizungumza na simu mara alimuona kijana kaingia chumbani kwake, na kumwambia awache simu na mtoto wake ambae alikuwa kampakata.

“Alinambia nimuache mtoto kama nataka usalama wangu, na nikaona mtoto siwezi kumuacha kwani sijajua kakusudia nini” alisema.