NA ABOUD MAHMOUD
WAZIRI wa Katiba na Sheria wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Palamagamba John Kabudi, ameomba kuwepo kwa mashirkiano baina ya Skuli ya Sheria Zanzibar na Skuli ya Sheria Tanzania bara.
Amesema mashirikiano hayo yatasaidia kujenga umoja na kupatikana mafanikio yanayotokana na ushirikiano katika nyanja mbali mbali ikiwemo masomo yenyewe.
Waziri Kabudi aliyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mafunzo kwa wajumbe wa baraza la kwanza la skuli ya sheria katika ukumbi wa Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mazizini nje kidogo ya mji wa Unguja.
“Ushirikiano wa kitaasisi ni mzuri na unaibua mambo mengi ya kimaendeleo, hapa nchini kwetu zipo skuli za sheria za Zanzibar na Tanzania bara, kama mtashirikiana mtaweza kufika mbali,” alisema Kabudi.
Alisema kwamba mashirikiano hayo yatajenga, kulinda mila na desturi za Tanzania ili lengo la skuli hiyo katika kutoa taaluma kwa wanafunzi wa sheria liweze kufikiwa.
“Ni jambo muhimu sana kulinda mila na desturi kwa sababu kama hatukufanya hivyo sasa hivi watoto wetu itakua hatukuwatendea haki kwa sababu hawajui tulipotoka,” alisema.
Aidha Kabudi alieleza kwamba kuanzishwa kwa skuli ya sheria visiwani humu kutasaidia wanasheria kuboresha kazi zao kwa wananchi wa Zanzibar kupitia msaada wa kisheria.
Alisema kutokana na wawekezaji kutoka mataifa mbali mbali kuja kuwekeza nchini watafaidika kutokana na kuwepo kwa wanasheria ambao wamepata taaluma kutoka skuli hiyo.
“Naamini kwamba kuanzishwa kwa skuli hii kutaleta mafanikio makubwa sana kutokana na wanafunzi kutoka mataifa mbali mbali duniani watakuja kusoma hapa,” alisema.
Naye Mkuu wa Skuli ya Sheria Zanzibar, Dk. Ali Ahmed Uki, alisema skuli hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari, 2022 ambapo masomo hayo yatasomeshwa katika Chuo cha Utawala wa Umma (IPA).
Uki alisema mpaka hivi sasa wanatarajia skuli hiyo kuanza na wanafunzi 100 ambao watasoma hapo kwa muda wa mwaka mmoja ambapo alifafanua kwamba masomo ya nadharia yatasomeshwa kwa muda wa miezi minne na vitendo watasoma kwa miezi minane.
Aidha Dk. Uki alisema lengo la kuanzishwa kwa skuli hiyo Zanzibar kumetokana na changamoto mbali mbali zinazowakabili wanasheria ikiwemo ya kufanya kazi zao bila ya kufuata misingi ya taaluma na maadili kama yanavyotakiwa.
Hivyo alifahamisha kwamba kuwepo kwa skuli hiyo kutasaidia kuondosha malalamiko hayo na wanasheria, mawakili, pamoja na mahakimu kufanya kazi kwa misingi madhubuti inayotakiwa.