NA MATHIAS CANAL, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema kuwa kumekuwa na mitazamo tofauti miongoni mwa wadau kuhusu sababu ya kuwepo kwa changamoto na matatizo sugu ya ushirika na namna ya kushughulikia na kutatua changamoto hizo.

Wadau wengi wa ushirika Tanzania bara wamekuwa na mtazamo kwamba changamoto na matatizo sugu ya ushirika nchini yanatokana na sababu mbalimbali na miongoni mwa sababu hizo ni mapungufu ya sheria inayosimamia sekta ya ushirika nchini, ambapo sheria hiyo ni ile ya Vyama vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa sasa serikali imekuja na muarobaini wa kutatua changamoto hizo.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua kikao cha wadau wazoefu wa ushirika kujadili mapendekezo na marekebisho ya sheria ya vyama vya ushirika Na 6 ya mwaka 2013.

Waziri Mkenda alisema kuwa kufuatia mtazamo wa wadau na dhamira ya kutatua changamoto sugu za ushirika zinazotokana na mapungufu ya sheria, mwaka 2019 serikali kupitia wizara ya Kilimo ilielekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanza mchakato wa kufanya mapitio ya sheria ya vyama vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.

Katika mkutano huo waziri Mkenda aliimpongeza mtendaji mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dk. Benson Ndiege kwa kufanikiwa kuwaalika wadau wote wazoefu katika kikao hicho kwa ajili ya kutoa maoni.

Kadhalika, waziri Mkenda aliitaka tume ya maendeleo ya ushirika pamoja na wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa maoni yatakayotolewa na wadau katika kikao hicho yanazingatiwa katika mchakato wa marekebisho ya sheria ya vyama vya ushirika unaoendelea.