MOGADISHU, SOMALIA

MAHAKAMA ya kijeshi nchini Somalia imewahukumu raia wawili wa kigeni wenye itikadi kali kwa kupigana wakiwa upande wa kundi la kigaidi la Al Shabab.

Mahakama hiyo mjini Mogadishu iliwahukumu Darren Anthony Byrnes kutoka Uingereza na Ahmad Mustakin Bin Abdul Hamid kutoka Malaysia kifungo cha miaka 15 jela, kwa kuwa wanachama wa al Shabab na kuingia Somalia kinyume cha sheria.

Ni raia wa kwanza wa kigeni wenye itikadi kali kuhukumiwa nchini Somalia kwa sababu ya uanachama wao kwa Al Shabab.

Waendesha mashitaka walisema Abdul Hamid na Byrnes waliingia Somalia ili kuunga mkono Al Shabab na kuharibu .

Wakili wao, Mohamed Warsame Mohamed alisema wanaume hao walikanusha uanachama wao katika kundi la Al Shabab na kudai kwamba walikuja Somalia kutembelea jamaa na marafiki.

Mohamed alisema, hakuna mashahidi wanaounga mkono utetezi wa serikali mahakamani.Alisema badala yake, serikali imetumia maelezo ya watu waliotoa ushahidi bila kuwepo mahakamani na madai kwamba washitakiwa walikiri kuwa wanachama wa Al Shabab.