NA MWANTANGA AME

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wiki iliyopita amefungua kikao kazi cha maofisa wa Jeshi la Polisi, na kuwataka kufanya marekebisho ya sheria mbali mbali za taasisi hiyo, ili kupunguza matukio ya kihalifu nchini yasitokee.

Rais Samia, katika kikao hicho alisema umefika wakati kwa Jeshi la Polisi, kukaa na wadau wengine kuangalia uwezekano wa kurekebisha Sheria zikiwemo ya kuweka watu mahabusu, pamoja na ile ya muda wa upelelezi.

Alitoa mfano mzuri wa Nchi nyingine ambapo mtu hakamatwi mpaka upelelezi utimie, lakini Tanzania kesi nyingi zinakwama Mahakamani kutokana na kucheleweshwa kwa upelelezi au kukosekana ushahidi na kubadilishwa majina kwa kuitwa kesi za kubambikiza.

Hali hiyo, alisema inachangia kuongezeka kwa takwimu kuwapo kwa idadi kubwa ya mahabusu jela, kwani hadi kufikia  Agosti 22, mwaka huu, wapo 15,194 idadi yao, ipo karibu sawa na wafungwa wapatao 16,542, ambao wapo waliokaa wiki moja, wiki mbili, miaka miwili na mitatu.

Alisema kila kesi inayoguswa imeonesha upelelezi haujakamilika, hali inayosababisha kubebesha mzigo mkubwa serikali, na amesisitiza, kama kesi haina mwelekeo watu watolewe na  zile ambazo wana uhakika upelelezi wake utatimia basi uharakishwe, ili kesi ziende Mahakamani.

Nafikiri wazo hili la Rais Samia lipo sawa, kwani tayari hivi sasa kumekuwa na lawama nyingi zinazotupiwa Jeshi la Polisi, juu ya kuwaweka watu ndani bila ya kujua hatma ya kesi zao, na mwisho wake huishia kufutwa vituoni ama Mahakamani kutokana na kukosa dhamana.

Baya zaidi ambalo lilikuwa likitokea ni kwa watuhumiwa kuwekwa ndani kwa siku ama wiki kadhaa katika vituo vya Polisi, bila ya kupewa dhamana, na ilipotokea kulalamikiwa hali hiyo ndio kidogo imepunguza msongomano katika vituo vya Polisi.