MOGADISHU, SOMALIA
RAIS Mohamed Farmajo wa Somalia amemvua madaraka waziri mkuu Mohamed Roble, hatua ambayo itakuza mpasuko wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili.
Rais Farmajo alisema kwenye taarifa yake kuwa alisitisha kwa muda madaraka ya waziri mkuu huyo ya kuwaajiri na kuwaondoa maofisa wa serikali nchini humo.
Farmajo, ambaye amekuwa na mgogoro na Roble kuhusu kuendesha shughuli za serikali alimshutumu waziri mkuu huyu kwa kufanya maamuzi ya haraka na ya upande mmoja bila ya kushauriana kwanza na Ikulu ya rais.
Pia alimkosoa Roble kwa kutotekeleza majukumu yake ya kuongoza mchakato wa uchaguzi, akisema maamuzi yake ya haraka yanaweza kusababisha misukosuko ya kisiasa na kiusalama nchini humo.