NA MASANJA MABULA

MDAU wa maendeleo na mfanyabishara, Mohammed Raza Hassanali amekabidhi msaada wa vifaa vya skuli wenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa skuli ya Pandani msingi na Wete sekondari.

Katika hafla hiyo Raza aliwashauri wafabiashara na wahisani wa maendeleo kutoa misaada yenye viwango ambayo itakidhi mahitaji ya walengwa na kuacha kutoa misaada isiyokuwa na tija kwa jamii.

Misaada iliyokabidhiwa na mfanyabiashara huyo ni meza 100, viti 100, seti mbili za komputa kwa skuli ya Pandani msingi na vitanda 50 na magodoro yake na mashuka 100, mito 50 na taulo 50 kwa skuli ya Wete sekondari na kuahidi kuendelea kusaidia sekta ya elimu.

Alisema elimu ni moja ya sekta ambazo zinahitaji kuendelezwa, hivyo atahakikisha anaunga mkono juhudi za serikali katika kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa wananchi.

“Nitaendelea kusaidia sekta ya elimu na sekta nyengine ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja ikiwemo pia sekta ya afya, maji na umeme”, alisema.

Aidha mfanyabiashara huyo aliwashauri wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa misaada ya vifaa vyenye ubora na ambavyo iwapo vikiwafikia wananchi vitakuwa na tija.

Baada ya kupokea msada huo, mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib aliahidi matokeo chanya katika mitihani ya kitaifa.

Alimuagiza mkuu wa wilaya kusimamia matumizi ya vifaa hivyo kwa kuwa karibu na walimu na wanafunzi ili vifaa hivyo viwe ni chachu ya mafanikio.

“Vifaa hivyo ni lazima viwe ni chachu ya matokeo chanya ya mitihani. Pia hakikisha unachukua hatua ikiwa ni Pamoja na kuvunja kamati za Skuli ambazo zitashindwa kusimamia na kutoa matokeo chanya”, aliagiza.