NA TATU MAKAME

MKOA wa Kasikazini Unguja, umepokea ujumbe wa wataalamu wa afya kutoka nchini Italia kwa lengo la kusaidia sekta ya afya mkoani humo.

Ujumbe huo ulifika Mkokotoni katika ofisi za Mkuu wa mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmoud, kujitambulisha baada ya shirika la Italian Agency Development Cooperation (IADC) kutaka kuimarisha mifumo ya sekta ya afya hapa zanzibar.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Ayoub alisema ujumbe huo pia ulitambulisha mradi wa afya unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2022 ambao utaimarisha mifumo ya kiafya, mawasiliano, vifaa vya afya na kuwajengea uwezo maofisa wa afya mkoani humo.

Aliweka bayana kua mradi huo wa miaka mitatu unatarajiwa kutekelezwa kwa muda ambapo utahusiasha kubadilishana uzoefu baina ya madaktari wa Zanzibar kwenda Italia na wale wa Italia kuja Zanzibar kwa lengo la kujifunza mambo yanayohusiana na afya ya binadamu.

“Mradi huu una manufaa makubwa sio kwa mkoa wetu pekee bali hata nchi nzima kwani mradi huu bila shaka utaleta mabadiliko katika sekta ya afya na kuimarisha uwezo kwa watendaji,” alieleza Ayoub.

Kiongozi wa ujumbe huo David Bonech,  alimuhakikishia Mkuu wa mkoa  kuwa  wapo tayari kutoa mafuzo kwa madaktari wa  Zanzibar ili kuimarisha utoaji wa huduma kama yalivyo malengo ya mradi huo.

“Wajibu wetu ni kushirikiana ili kuleta mabadiliko kwa mujibu wa sera ya afya ya Zanzibar na Shirika la Afya duniani (WHO) la kupeleka huduma za matibabu mikoani na vijijini.

Ujio wa maofisa wa Shirika la IADC ni mwendelezo wa jitihada za serekali kuhakikisha Zanzibar na Tanzania zinapata maendeleo katika sekta ya afya ambapo  jumla ya Euro  milioni 1.250 zimetengwa na shirika hilo kwa ajili misaada ya Tanzania.