LONDON, England
IKIWA ni baada ya miaka 12 tangu Cristiano Ronaldo aondoke Manchester United, nyota huyo wa dunia amerejea kwa kishindo Old Trafford.
United walikua uwanjani kuwaalika Newcastle United katika mchezo wa nne wa Ligi Kuu ya England. Mchezo huo ulikuwa umezikutanisha timu mbili zenye historia kubwa na heshima kwenye soka la England.

Baada ya kukamilisha usajili wake kurejea United, huo ulikuwa ni mchezo ambao mashabiki walimpokea rasmi Ronaldo na hakika, “CR7 is back!”.
Ushindi wa magoli 4-1 wa United, ulichangiwa na magoli mawili ya CR7, Bruno Fernandez na Jesse Lingard huku goli la Newcastle United likipachikwa na Manquillo.
“Sikutarajia kufunga magoli mawili,” gwiji huyo wa Ureno, alisema.
“Nilitarajia moja, lakini sio mawili. Ulikuwa wakati wa kushangaza”.

Ronaldo alifunga magoli 118 katika michezo 292 akiwa na United kati ya mwaka 2003, alipojiunga akiwa kijana, na 2009 alitimkia Real Madrid kwa ada ya pauni milioni 80.
Katika miaka 12 iliyofuata, alifunga mabao 551 akicheza Real na Juventus kabla ya uhamisho wa mshangao wapauni milioni 12.8 kurejea United siku ya mwisho ya usajili.
Moja ya ushindi wake wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja ya tuzo zake tano za ‘Ballons d’Or’ ilikuja wakati wake huko England.
Ushindi huo uliifanya United ikae kileleni ikifikisha pointi 10 sawa na Chelsea ambayo nayo ilishinda magoli 3-0 mbele ya Aston Villa.

Wakati huo,inaelezwa kiungo Paul Pogba, atabakia United kufuatia kurejea kwa Ronaldo.
Pogba alikuwa akitajwa kutaka kujiunga na Real Madrid na nyota huyu wa Ufaransa bado ana mkataba na United ambao unafika tamati mwisho wa msimu huu.
Meneja, Ole Gunnar, amenukuliwa akisema nyota huyo haondoki United.
Lakini, ikiwa nyota huyo hatofanya maamuzi mapema kama anataka kusalia United na kusaini mkataba mpya, kuna uwezekano wa kuwekwa sokoni katika dirisha la mwezi Januari ili United wasiweze kumpoteza bure.

Kurejea kwa Ronaldo kumerejesha nguvu na motisha United, na klabu ina malengo makubwa, na hakuna shaka kuwa huenda Pogba asiamue kuondoka na kuendelea kupambana katika morali iliyopo sasa United ili waweze kushinda mataji muhimu.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, Paris Saint Germain na Juventus, zinavutiwa na saini ya Pogba, zikipambana na Real Madrid ambao pia wanaisaka saini yake.

Madrid wanamhitaji zaidi nyota wa aina ya Pogba, wakati Toni Kroos akiwa nje kwa majeraha huku Luka Modric akiwa anafikisha miaka 36 sasa.
Lakini,Casemiro amekubali kusaini mkataba hadi 2025 na Fede Valverde naye hadi 2027, huku Eduardo Camavinga akiwasili akitokea Rennes na Pogba anaweza kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Madrid. (Goal).