LISBON, Ureno
CRISTIANO Ronaldo amevunja rekodi ya ufungaji katika michezo ya timu za taifa za wanaume baada ya kufunga magoli mawili katika ushindi muhimu wa 2-1 walioupata Ureno dhidi ya Jamhuri ya Ireland kuwania kufuzu Kombe la Dunia uliochezwa juzi.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36, alifunga magoli hayo kwa kichwa na kufikisha gali 28 ya kichwa ngazi ya taifa, akivunja na kuweka rekodi yake akifikisha magoli 110 na 111.

Awali rekodi ya kufunga magoli mengi ilikuwa inashikiliwa na Ali Daei ambaye alifunga magoli 109 akiwa na Iran kati kati ya mwaka 1993-2006. Rekodi hiyo ya magoli ilifikiwa na Ronaldo baada ya kufunga mabao mawili kwenye mechi dhidi ya Ufaransa kwenye michuano ya Euro 2020.

Ronaldo ambaye mwanzoni mwa wiki hii alikamilisha kujiunga na Manchester United pia amefikia rekodi ya beki wa zamani wa Real Madrid, Sergio Ramos ya kucheza mechi nyingi, ambapo Mreno huyo amecheza mechi 180.

Ronaldo mwenye umri wa miaka 36 amrejea Manchester United baada ya klabu hiyo kufikia makubaliano na Juventus juu ya usajili huo.

Mshambuliaji huyo ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d’Or’ mara tano na mataji makubwa 30, katika maisha yake kisoka.

Mataji hayo ni Klabu Bingwa Ulaya (5), mataji 4 ya FIFA kwa ngazi ya klabu, makombe saba ya Ligi Kuu ya England, Hispania na Italia pamoja na Kombe la Ulaya akiwa na timu yake ya taifa ya Ureno.Katika kipindi chake akiwa na United, alipachika mabao 118 katika michezo 292. (Goal).