ZASPOTI
BEKI wa kati wa Ujerumani, Antonio Rudiger, amechagua kutoongeza kandarasi yake Chelsea zaidi ya msimu ujao wa kiangazi.
Miamba ya Bayern Munich na Real Madrid inatajwa kumfukuzia beki huyo mwenye umri wa miaka 28.
Mkataba wa Rudiger utamalizika mwishoni mwa kampeni ya sasa, na Chelsea inajaribu kutaka kumbakisha Stamford Bridge. Klabu hiyo imetoa euro milioni 6.5 kwa mwaka ili kuongeza mkataba mpya, lakini, ameomba euro milioni 10, akiacha suluhisho likiwa bado liko mbali.

Sasa wakala wa Rudiger anafanyakazi ya kutafuta suluhisho mahali pengine. Akiwa Chelsea tangu 2018, wakati aliposainiwa akitokea Roma, Mjerumani huyo amepiga hatua kubwa mbele katika misimu ya hivi karibuni na hasa tangu kuwasili kwa Thomas Tuchel.
Real Madrid wanatafuta beki wa kati kwa ajili ya msimu 2022/23 na ingawa mtazamo wao unabakia kwa wachezaji wachanga, kila wakati wamekuwa wakizingatia fursa za soko kwa njia ya wachezaji wenye viwango waliokuwa huru, kama ilivyoonekana kwa kumsaini, David Alaba siku za nyuma majira ya joto.

Los Blancos watalazimika kupima mambo yao kifedha, lakini, wanaweza kuanza kumpigia hesabu Rudiger aungane na Alaba, Nacho Fernandez na Eder Militao huko Estadio Santiago Bernabeu msimu ujao wa joto.
Chelsea haijafanikiwa kukamilisha mazungumzo ya mkataba mpya wa Rudiger huku ikiripotiwa inakutana na kikwazo, katika jitihada za kumshawishi nyota huyo kusaini mkataba mpya.

Kwa mujibu wa chanzo kimoja huko England, ofa ya hivi karibuni ya Chelsea ya mkataba mpya ilikwenda tofauti huku maboresho zaidi yakishauriwa kufanyika kwenye mkataba huo.
Mbali ya Real na Bayern klabu za Paris Saint-Germain, Juventus na Atletico Madrid zinasikilizia hatma ya Rudiger na Chelsea.
Pia Tottenham Hotspurs, ndiyo wanaotajwa kuwa wapinzani pekee wa Ligi Kuu ya England wanaojaribu kuonesha nia ya kumtaka nyota huyo. Awali Spurs walishajaribu kuinasa saini yake.

Wakati seke seke la mkataba mpya wa Rudiger likiendelea, mpaka sasa ameshacheza zaidi ya mechi 150 na Chelsea tangua alipowasili klabuni hapo.
Wakati huo huo, Chelsea ipo tayari kumuuza kiungo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 30, N’Golo Kante, msimu ujao.
Lakini hilo litategemea iwapo kocha Thomas Tuchel, ataona haja hiyo kutokana na kiwango bora cha mchezaji huyo kwa sasa.
Wiki iliyopita, Tuchel, alimtaja Kante kama mchezaji aliyeleta mabadiliko katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Tottenham.

Kante alitokea benchi kuchukua nafasi ya Mason Mount katika kipindi cha pili cha ‘dabi’ hiyo ya London na kuisaidia ‘Blues’ kuibuka na pointi tatu muhimu.
Kante aliifungia timu yake goli la pili na kumvutia kocha huyo wa Ujerumani kwa uchezaji wake katika mchezo huo.
“Alicheza kwa sehemu kubwa. N’Golo ni N’Golo, ni wa kipekee, wa aina yake na kuwa naye uwanjani hufanya tofauti kubwa kwa kila kitu”.
“[N’Golo] Ni mchezaji bora. Ukiwa na N’Golo, una kitu kila mtu anatafuta.“Ni mtu wa kipekee … ni mzuri”. (Marca).