KABUL, AFGHANISTAN

SAFARI za ndege za kimataifa zimeanza tena nchini Afghanistan, ikiwa hatua muhimu kwenye juhudi za serikali mpya ya Taliban kurejesha hali ya kawaida baada ya kutwaa madaraka mwezi uliopita.

Ndege ya shirika la ndege la Qatar iliondoka kuelekea Doha ikiwa na abiria 113, wakiwemo raia wa Ujerumani, Marekani, Canada na Uingereza.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Ned Price, alithibitisha kuwa raia kumi na wakaazi 11 wa kudumu wa nchi hiyo walikuwemo kwenye ndege hiyo.

Mjumbe maalum wa Qatar nchini Afghanistan, Mutlaq bin Majed al-Qahtani, alisema safari hii ni ya kawaida na si sehemu ya kampeni ya kuwahamisha watu wanaotaka kuikimbia Afghanistan.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani aliwashukuru viongozi wa Taliban kwa kusaidia kwenye kuufungua tena uwanja mkubwa wa ndege wa Kabul.