NA MADINA ISSA

FAMILIA ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Mpendae, marehemu Salim Turky, imeanzisha taasisi ya ‘Salim Turky Foundation’ kwa lengo la kumuenzi na kuendeleza mambo aliyoaanzisha na kuyaahidi wakati wa uhai wake.

Mbunge wa sasa wa jimbo hilo ambae ni mtoto wa marehemu Salim Turky, Taufik Salim Turky, alisema kuwa ‘foundation’ hiyo imejikita katika masuala mbali mbali ikiwemo kutoa misaada kwenye upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kumalizika dua iliyoandaliwa na familia hiyo nyumbani kwao Mpendae, iliyowashirikisha watoto yatima waliomo jimboni humo, alisema taasisi hiyo imeanza kazi kwa kutoa mchango katika ujenzi wa mabweni ya Chuo cha Mwalim Nyerere kampasi ya Karume, Zanzibar.

Aidha alisema kuwa ‘foundation’ yao imepanga kujenga nyumba kwa ajili ya watoto yatima ambapo nyumba hizo zitajengwa katika visiwa vya Zanzibar.

“Sio kama tutaweka makaazi tu, bali tutawapatia elimu watoto hao pamoja na kuwawezesha kimaisha kwa kuwapa elimu ya dini na dunia ili nao wajihisi ni miongoni mwa watoto na wenye wazazi wao,” alisema.

Alifahamisha kuwa wakati wa uhai wa baba yao alikuwa na ndoto ya kuwasaidia watoto yatima ambapo alikuwa akitoa misaada mbalimbali ili kuona na wao wanakuwa kama watoto wengine.

Sambamba na hayo, alisema katika kufanikisha hilo, wamebuni miradi mbali mbali ili kuona lengo hilo linafikiwa kuwasaidia watoto hao na kuendeleza kutoa misaada kuwasaidia wazee, ujenzi wa misikiti pamoja na suala la huduma za maji safi na salama katika jimbo lao.

Alisema, huko utakuwa utaratibu wa kila mwaka kwani marehemu aliacha pengo kubwa sio Kwa familia tu basi hata Jimbo kwa ujumla.

“Huu utakuwa utamaduni wetu katika na tutahakikisha kila mwaka tunamuombea dua mzee wetu kwani katika uhai wake alikuwa nasi bega wa bega katika kututatulia changamoto zetu zilizopo katika jimbo,” alisema.

Sambamba na hayo, alitoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo na majimbo jirani kujitokeza katika kupiga chanjo ya ugonjwa wa uviko 19 kwani ugonjwa huo umekuwa ukiathiri maisha ya watu na uchumi ulimwenguni.