NA SAIDA ISSA, DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwakani ina lengo la kufahamu idadi ya watu, mahali walipo, jinsia, rika, elimu, ajira, shughuli, makazi yao, hali zao.

Samia alieleza hayo jana katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwenye hafla ya uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani.

Alisema taarifa hizo zitasaidia kufahamu wastani wa ongezeko la idadi ya watu katika nchi na pia hali ya uhamiaji kutoka vijijini kwenda mijini na kuwezesha nchi kutambua hatua mbalimbali za kimaendeleo.

Alifahamisha kuwa sensa inasaidia serikali kufanya maamuzi kuhusu ugawaji wa rasilimali za taifa na kupeleka huduma za jamii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo yao kulingana na idadi ya watu na mahitaji.

“Zoezi hili si geni kwetu limekuwepo duniani tangu karne na karne katika kuthibitisha hilo suala la sensa linatambulika kwenye dini zetu zote na tumesikia viongozi wetu wa dini hapa wakiyasema vizuri sana”, alisema Samia.

Samia alisema mbali na kupitia madodoso ya sensa ya mwaka 2022, sensa itawezesha kutambua idadi ya majengo na mahali yalipo, kufahamu hali ya mahitaji ya makazi na kupanga mitaa kupitia anuani za makazi ambazo zitachochea benki kutoa mikopo na kupunguza viwango vya riba.

Aliwapongeza viongozi wa serikali, dini na vyama vya siasa kusisitiza wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo la sensa ya watu na makazi, ambapo pia aliwasihi viongozi wa dini wasisahau kuzungumzia suala la sensa kila watakapotoa mahubiri kwa waumini wao.

Samia aliishukuru na kuipongeza kamati kuu ya taifa ya sensa kwa kukamilisha mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji sensa mapema na kuwataka kwenda kuutekeleza.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. Phillip Mpango aliwataka watanzania wakati utakapofika wa kufanya sensa, kila mmoja ajitokeze kuhesabiwa kwani taarifa za sensa zina umuhimu kwa maendeleo ya wananchi.