Ataka uchimbaji unaozingatia manufaa na tija

Wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali yake

NA MWANDISHI WETU, MERERANI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema uwazi juu ya yanapotoka madini ya Tanzanite utajulikana baada ya kukamilika kwa filamu ya vivutio vya utalii Tanzania kuwekwa hadharani.

Rais Samia, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mirerani, mkoa wa Kilimanjaro akiwa njiani kuelekea katika machimbo ya madini hayo ikiwa ni sehemu ya utayarishaji wa filamu hiyo inayoitwa ‘Royal Tour’.

Filsmu hiyo inayolenga kutangaza vivutio vya utalii, mila na desturi za Watanzania uzinduzi wake utafanyika nchini Marekani na kuoneshwa katika vituo mbali mbali vya televisheni ulimwenguni.

Alisema Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa sekta ya utalii, imeamua kufanya filamu hiyo kwa dhamira yakuitangaza nchi ili dunia izidi kuijua vyema Tanzania na mazingira yanayoizunguka.

Alisema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikizalisha madini hayo lakini kulikuwa na utata juu ya mahali yanapotoka baada ya nchi nyingi kujinasibu nayo.

“Filamu hii itaijulisha dunia Tanzanite inapotoka, inapochimbwa, inapoongezwa thamani na yanapouzwa, ikiwa ni hatua ya kuondoa utata wa baadhi ya mataifa kujisingizia kuzalisha madini haya,” alieleza Samia.

Aliongeza kuwa hatua hiyo, itachangia kuongeza thamani ya madini hayo katika soko la dunia na kuwataka wachimbaji kuwa na uzalishaji utakaowapa faida katika kazi yao na kuimarisha uchumi kwa muda mrefu.

Aidha Rais Samia, alisema madini hayo yanapouzwa kiholela yanashusha thamani yake na yanatakiwa kuuzwa kwa mpangilio maalum.

Kutokana na hilo, Rais Samia aliwaomba wachimbaji katika migodi kuhakikisha wanazingatia vigezo vya msingi vitavyoongeza thamani ya madini yao, na sio kufanya uchimbaji wa ovyo.

Aliwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono ili kuifanya Tanzania iendelee kubakia na amani, huku ikiwa na utawala bora na siasa safi, ikiwa ni hatua itayowafanya  wawekezaji kuja hapa nchini kuwekeza.