Asema rais wa sasa yupo kwa kudra ya Mungu

NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wanawake wa Tanzania ndio watakaomuweka madarakani rais mwanamke ifikapo mwaka 2025, kauli ambayo ilisababisha shangwe kubwa.

Samia alieleza hayo jana katika ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya demokrasia yaliyoandaliwa na asasi za ULINGO na wanawake wajasiriamali.

Samia alisema hivi sasa mwanamke yupo madarakani kwa mujibu wa kikatiba na kudra ya Mwenyezi Mungu, hivyo wajipange ili kumuweka katika kiti hicho rais mwanamke ifikapo mwaka 2025.

Aliwaeleza wanawake kwamba wakifanya vitu vyao vizuri, wakijipanga na kushikamana vizuri wataweza kumuweka rais mwanamke mwaka 2025, na baada ya ushindi watakutana katika ukumbi huo kwa ajili ya kujipongeza na kufurahia.

“Wameanza kutuchokoza kuandika kwenye vigazeti Samia hatasimama nani kawaambia… wanawake bado hatujamuweka rais mwanamke, rais huyu amekaa kwa sababu ya kudra ya Mungu na matakwa ya katiba…”, alisema Samia.

Aidha aliongeza kuwa, “tulichochangia sisi na dada zetu na mama zetu ni ile kusukuma hadi mwanamke akawa Makamu wa Rais ule ndio mchango mkubwa tulioufanya wanawake, lakini kufika hapa kama isingekuwa kudra ya Mungu ingekuwa ngumu sana”, alisema.

Akigusia demokrasia alisema Novemba 8, 2007 Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio kila ifikapo Septemba 15 ya kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya demokrasia, ambayo ikiwa na lengo la kutoa fursa kwa wadau wa kutafakari ukuaji wa demokrasia.

Alifahamisha kuwa demokrasia ni dhana pana, ambayo inahusisha masuala kadhaa muhimu yakiwemo uwepo wa uhuru katika nchi, wa kutoa maoni, uhuru wa habari, uhuru wa kujenga na vikundi.