PYINMANA, MYANMAR

SARAFU ya Myanmar imeshuka thamani tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi mwezi Februari, na kuathiri mno maisha ya watu kwa kuwa bei za bidhaa kutoka nje zinapanda.

Benki kuu ya nchi hiyo sasa inaweka kiwango cha kubadilisha fedha cha kati 1,921 kwa dola.

Hiyo ina maana kuwa sarafu ya Myanmar imeshuka kwa zaidi ya asilimia 40 dhidi ya dola tangu jeshi lichukue madaraka.

Lakini thamani ya kyat imeshuka zaidi kwenye taasisi za ubadilishaji fedha zilizo mitaani.

Dola ilikuwa inauzwa karibu kyat 2,700 katika mji mkubwa wa Yangon.

Inaaminika kwamba idadi inayoongezeka ya wananchi wanaona ni bora kuwa na sarafu ya Marekani kutokana na hofu za siku zijazo.

Kushuka kwa sarafu ya kyat kumesababisha bei za bidhaa zinazoingia nchini humo kutokea nje kupanda.

Ripoti zinasema bei za mafuta zimeongezeka maradufu ikilinganishwa na kabla ya kutokea kwa mapinduzi na bei za dawa nazo pia zinapanda.

Benki kuu imeongeza kwa muda udhibiti ili kujaribu kusimamia viwango vya ubadilishaji fedha na mara kwa mara iliingilia soko ili kuimarisha sarafu yake.Lakini kuna uwezekano mdogo wa kuzuia ushukaji wa sarafu hiyo.