NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zimeshauriwa kuendelea kuwasaidia vijana kujiendeleza na elimu ya juu ili nchi ipate wataalamu.

Mhasibu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania (SAUT), Ananias Aloys Rutambue, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya fursa zinazotolewa na chuo hicho katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni.

Alisema pamoja na serikali kuwasaidia vijana na wafanyakazi wa taasisi za serikali kwa kuwalipia gharama za masomo, bado jitihada zinahitajika kuwashajihisha vijana kusoma masomo ya elimu ya juu.

Alisema hatua hiyo itawawezesha vijana kujiendeleza katika vyuo nchini na kufikia malengo yalikusudiwa.

“Ni vyema taifa likawekeza kwa vijana ili na wao wathamini juhudi zinazochukuliwa na serikali zote mbili katika kuhakikisha wanatumia ipasavyo fursa ya kujiendeleza,” alieleza Rutambue.

Akizungumzia fursa ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Rutambue alisema baadhi ya watu wanapomaliza masomo na kupata ajira wanakataa kulipa mikopo jambo ambalo sio sahihi na kinyume na sheria.

“Serikali zetu zote mbili zina lengo moja la kutoa mikopo kwa ajili ya watu kupata elimu ya juu, niwaombe wale wanaomaliza na kuajiriwa, warejeshe mikopo ili wengine waweze kuitumia vyema fursa hiyo,” alisisitiza.