NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdalla Hussein Kombo, amesema wizara yake inamaliza maandalizi ya sera na mkakati matumizi ya bahari katika kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu.

Hayo aliyaeleza huko katika ukumbi wa ZURA, wakati wa mafunzo kuhusu dhana ya uchumi wa buluu na mpango wa matumizi ya bahari kwawajumbe wa kamati za fedha na bajeti za Baraza la Wawakilishi, Zanzibar.

Alisema kwamba katika utekelezaji wa hilo wameanza kushirikisha wadau mbali mbali wakiwemo viongozi wa taasisi za seriksali na binafsi na wananchi ili kupata maoni yao kwa kuanzia Unguja na baadae wataenda Pemba.

Aidha pamoja na hatua hiyo, pia wameanza kukusanya taarifa na baada ya hapo wanakwenda katika mpango wa kupanga matumizi ya namna gani sekta zitakazokusanyika kwa pamoja ili kuboresha mpango wenyewe.

Hata hivyo alisema kwamba mpango wenyewe lazima waeleze wanachotaka kukifanya kwenye uchumi wa buluu na vipaumbele wanavyotaka kuviweka katika vitega uchumi na baadae wapange uvuvi unaotakiwa ufanyike, maeneo ya kufanyika kwake pamoja na vitu vyengine.

Hivyo alisema kwamba wakimaliza sera hiyo na mkakati hapo ndipo watakapoelewa Serikali ya awamu ya nane inaelekea wapi kwenye uchumi wa buluu.

Katika mafunzo hayo wajumbe hao walitaka kujua kama kuna tathmini iliyofanyika kabla ya kuanza utekelezaji wa dhana hiyo katika eneo la bahari kuu ili kujua matumizi kwa ujumla.

Awalieleza kuwa kuna umuhimu wa kutambua viashiri vya madhara yatakayojitpokeza na kuweka mkakati utakaokabili madhara hayo ili yasiaathiri jamii.

Mwakilishi wa jimbo la Pandani Prof. Omar Faki Hamad, aliwataka wataalamu wanaoandaa sera na mkakati huo kuwa makini katika mfumo huo ili kusitokee misukumo katika utendaji kazi zao na kuishauri serikali iwe na idara itakayojihusisha na kazi hiyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani, Yahya Rashid Abdulla, alisema suala zima la uchumi wa buluu na mpango wa matumizi ya bahari pamoja miongozo ni lazima kuwepo na mkakati imara ambao ndio utakaofanikisha utekelezaji wake.