NA ABOUD MAHMOUD

KUWEPO kwa  sera na sheria zinazohusiana na watu wenye ulemavu Tanzania Bara na Zanzibar zinazoenda na wakati ni fursa muhimu ya kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya  taasisi zinazosimamia ustawi na maendeleo ya kundi hilo nchini.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak, alieleza hayo alipokua akifungua kikao cha pamoja kati ya wajumbe wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu na ujumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tanzania bara.

Alisema mkutano huo utakuza ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa watendaji katika sekta zinazohusika na watu wenye ulemavu jambo litakalosaidia kuziendesha vyema hasa katika upande wa ujenzi wa mashirikiano ya kimaendeleo na jumuiya za kimataifa.

“Baada ya kikao hiki ni matarajio yetu kuongezeka kwa ufanisi na kufikia malengo kwa taasisi zetu hizi mbili ya hapa Zanzibar na ndugu zetu wa Tanzania Bara ambapo tunashirikiana na pia kujifunza ili yale malengo na mafanikio tunayoyataka yapatikane,” alisema.

Shajak alieleza vikao kama hivyo ambavyo vitakua endelevu na kufanyika kwa mwaka mara moja vitahakikisha wenye ulemavu Tanzania wanapata stahiki zao ambazo zinakubaliana kwa pande zote mbili.

“Watu wenye ulemavu wanauhitaji maalum ili waweze kutekelezewa kwa mujibu wa hali zinavyokwenda lakini pande zote mbili zitizame ubora wa mahitaji hayo kwa kila upande ili tuweze kwenda vizuri,”alifafanua.

Sambamba na hayo Katibu Mkuu huyo alisema kikao hicho kijenge mahusiano ya karibu yataweza kuzungumzia lugha moja ambayo itasababisha kupiga hatua kubwa kutoka walipo na kufikia sehemu nyengine.

Nae Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Jamal Adam, alisema kupitia vikao vya mashirikiano watendaji wa taasisi hizo watapata kutathmini utendaji wao na kuibua mambo ambayo yatazisaidia taasisi hizo kufikia maendeleo.

“Tumekuja kufanya kikao cha pamoja na hapa leo, tumejifunza mambo mengi ikiwemo njia bora ya kukusanya takwimu za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya shehia jambo ambalo sisi hatuna hivyo tunaenda kulifanyia kazi,”alifafanua Jamal.