NA LAYLAT KHALFAN

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema taratibu zote za kisheria zilifuatwa katika mchakato wa kupatikana kwa jengo lililotumika kupima na kutoa majibu ya virusi vya corona.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora, Haroun Ali Suleiman, alieleza hayo wakati akitoa taarifa kuhusu hoja ya ukodishwaji wa nyumba ya kupima maradhi ya corona.

Haroun alitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu wa Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, katika ukumbi wa baraza la Wawakilishi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema jengo hilo lilihitajika kutumika kwa muda wa miezi sita ili kupisha matengenezo yaliyokuwa yakifanyika katika jengo la wizara liliopo Lumumba.

“Serikali imeridhia mchakato wa dharura wa kumpata mzabuni kwa mujibu wa sheria ya manunuzi na uondoshaji wa mali za umma,” alisema waziri Haroun.

Haroun ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Makunduchi, alisema kwa sasa huduma zote zinaendelea kutolewa katika jengo la Lumumba lililofanyiwa ukarabati na wananchi wanaendelea na huduma hiyo bila ya usumbufu.

Alisema kutokana na sababu hizo, wizara ilimchagua mzabuni ambaye ni Rahisi Solution Company LTD kutokana na uwezo mkubwa wa kuweka na kuendesha mifumo ya aina hiyo hapa nchini.

“Mzabuni huyu alishawahi kufanya kazi za kutengeza mifumo katika taasisi mbali mbali za serikali ikiwemo Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ambayo iliingia mkataba na kampuni hiyo kwa uwekaji mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya usajili na upimaji wa virusi vya uviko 19 kwa muda wa miaka miwili kuanzia Mei 21, 2021 hadi Mei, 2023,” alisema.

Akitaja mambo yaliyobainika katika jengo lililokuwa likitumika kwa kupima na kutoa majibu ya virusi hivyo Mazizini, alisema jengo hilo lilipatikana baada ya Wizara ya Afya kutafuta eneo linaloendana vyema na utoaji wa huduma hizo kwa kutilia maanani suala zima la biashara ya utalii nchini.

Alisema na ndio sababu ya msingi ya kutafuta wazabuni watatu kwa njia ya dharura kama ilivyoelekezwa na kifungu 71 (3) (a)(b) cha sheria ya ununuzi na uondoaji wa mali ya umma nambari 11 ya mwaka 2016.