NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mwigulu Lameck Nchemba jana ametia saini marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya kieletroniki za kutuma na kutoa fedha za mwaka 2021 na kupunguza viwango vya tozo za miamala hiyo kwa asilimia 30.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja ilieleza kuwa waziri huyo amechukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Julai 19 mwaka huu.

Katika maelekezo yake hayo, Samia aliwataka waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Lameck Nchemba na waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile kupitia upya tozo za miamala ya simu baada ya kusikia kilio cha wananchi kuhusu tozo hizo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa serikali ilifanya majadiliano na watoa huduma za simu ambao nao wameridhia kupunguza viwango vya tozo wanazotoza katika miamala ya kutuma na kutoa fedha kati ya mtandao na mtandao mwingine kwa asilimia 10.

Aidha Benny Mwaipaja alisema viwango vilivyopunguzwa vitatangazwa rasmi katika tangazo la serikali leo Septemba mosi.

Alisema kuwa serikali inaamini kuwa uamuzi huo utatoa nafuu kwa wananchi na kuiwezesha kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyokusudiwa wakati tozo hizo ziliporidhiwa na kupitishwa na bunge la bajeti la mwaka 2021/2022.

“Ni imani ya serikali kwamba wananchi wataunga mkono uamuzi huu kwani tozo hizo zimeanza kuleta manufaa makubwa kwa wananchi ikiwemo kiasi cha shilingi bilioni 48.4 zilizokusanywa hivi karibuni ambazo zimeelekezwa katika kujenga vituo vya afya 150 na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 560 nchi nzima”, ilieleza taarifa hiyo.