NA MADINA ISSA

WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, ameziagiza Manispaa, Mabaraza ya miji na Halmashauri kuwasilisha ofisini kwake taarifa za makusanyo ya mapato ya kila mwezi.

Akizungumza katika kikao kilichowashirikisha Makaimu Wakurugenzi na maafisa mipango, kikao ambacho kilifanyika ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar, alisema ni vyema kuwasilisha ripoti za fedha kama wanavyowasilisha katika vikao vyengine kwa kila mwezi.

Alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kuweka mkazo katika ukusanyaji wa mapato katika taasisi zao wanazozisimamia ili lengo liweze kufikiwa kuendana na kiwango kinachotakiwa kukusanywa.

“Wizara itahitaji kujua kila mwezi taasisi hizi zimekusanya fedha kiasi gani pamoja na matumizi wanayotegemea kufanya,” alieleza Masoud.

Aidha alifahamisha kuwa utaratibu huo utawezesha kutambua makadirio na kiwango cha ukusanyaji wa tozo na mapungufu yanayojitokeza ili kuyafanyia marekebisho.

Alisema serikali za mitaa zinatakiwa kuchangia sehemu ya mapato ya serikali, hivyo ni lazima kuwe na ufuatiliaji wa kutosha ili kuweza kufanikisha mipango hiyo.

“Tunapokwenda hamutokusanya tu halafu zikabakia kuwa taarifa zenu, tuliwahi kusema huko nyuma kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 serikali za mitaa tunatakiwa kuchangia kwa asilimia 0.8 ambayo ni wastani wa shilingi bilioni 15 kwa mwaka,” alisema.