NA MWANAJUMA MMANGA

WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Omar Said Shaaban, ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Maendeleo ya viwanda vidogovidogo na vya kati (SMIDA) kufuata sheria, kanuni, miongozo na sera ya viwanda ili kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Shaaban aliyasema hayo wakati akizindua bodi ya wakala huo Maruhubi na kusema kufanya hivyo kutapunguza malalamiko ya wajasiriamali wanaozalisha bidhaa hapa nchini na wanaingiza kutoka nje kukwepa kulipa kodi.

Aidha aliitaka bodi hiyo kusimamia vyema majukumu yao ili kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wadau wake na kuihakikishia kuwa itakuwa huru.

“Bodi hairuhusiwi kuingilia majukumu ya watendaji bali ni wajibu wao kusimamia mipango na malengo ya serikali katika wakala ili malengo ya kuanzishwa kwake yaweze kufikiwa,” alisema Shaaban.

Alisema SMIDA inatakiwa kuweka mazingira yatakayowatengeneza wajasiriamali ambao watapiga hatua ya maendeleo katika kazi zao na kuchangia uchumi wa nchi.

Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo, Juma Hassan Reli, alisema kuwa bodi hiyo itahakikisha inafanyakazi ipasavyo ili kufikia azma ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wakiwemo wajasiriamali mbali mbali nchini.

“Niwaombe sana wenzangu tukafanye kazi kwa mujibu wa sheria zilizowekwa ili lengo la serikali ya awamu ya nane liweze kufikiwa” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa SMIDA, Soud Said Hassan, alisema changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kwa sasa zinaweza kuwa sababu zinakazopelekea kutofikiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo na kuomba zipatiwe ufumbuzi.