NA MWANTANGA AME, RUVUMA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeutaka uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuanza kununua mahindi ya wakulima yaliyokwama kwa zaidi ya mwenzi mmoja sasa.
Agizo hilo lilitolewa na Katibu wa halmashauri kuu ya ccm taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, baada ya kikao cha dharura na kundi la wakulima zaidi 243 waliolalamikia hali hiyo.
Wakulima hao walieleza kuwa, mahindi hayo yamekaa kwenye ghala la kuhifadhi mahindi kwa zaidi ya mwezi bila bidhaa zao kununuliwa licha ya serikali kutoa fedha.
Nasoro Nyoni anasubiri mahindi yake kununuliwa alisema hawajui hatma ya mahindi yao kwa kuwa wanapoteza muda mwingi kufuatilia malipo yao bila muafaka.
Alisema wamepatiwa taarifa ya serikali kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mahindi lakini kwenye utekelezaji hakuna.
“Nipo hapa tangu Agosti 15, mwaka huu nasubiria mahindi yangu yanunuliwe na yanavyochelewa yanaanza kuliwa na mchwa na pia tunapoteza muda mwingi kukaa hapa,” alisema Nyoni.
Naye Saimon Rwiga, alisema ana mwezi tangu ayalete mahindi yake na anashindwa kuondoka kwa kuwa anasubiria malipo yake, ili aweze kufanya shughuli nyingine.
Pumziko Philemon, alisena anachokiona ni kwamba serikali haikuwa na hela ya kununua mazao hali ambayo imesababisha usumbufu unaoendelea.
Alisema awali zilikuwa tani 1,470 za mahindi yakauzwa tani 1,000 na kubaki tani 470 ambazo ziliuzwa kwa wale wenye mahindi kuanzia magunia 80.