NA MWANTANGA AME, RUVUMA

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya taifa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Shaka Hamdu Shaka, ametoa shilingi milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chuo cha Emanuel Nchimbi na kuwataka wahandisi waliopewa kazi ya ujenzi huo kusimamia vyema na kukamilisha kwa wakati.

Shaka alitoa kauli hiyo alipotembelea miradi ya ujenzi wa madarasa katika skuli za Wilaya ya Songea mjini ikiwemo skuli ya msingi ya Amani , chuo cha Emanuel Nchimbi kunapojengwa bwalo.

“Ni lazima wahandisi mliopewa kazi za ujenzi wa madarasa haya mjipange na kuhakikisha miradi yote inakuwa na viwango vinavyokubalika na sio kuiripua,” alieleza Shaka.

Alisema serikali imeamua kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kujenga madarasa ikiwa ni hatua itayopunguza kuwapo kwa msongomano madarasani.

Alisema haitapendeza kuona serikali inatoa fedha hizo kwa ajili ya kuwawekea mazingira bora wanafunzi lakini waliopewa kazi ya ujenzi wakatumia viwango vya chini katika kazi zao.

“Angalieni hapa katika hii shule milango iliyowekwa zamani ni mizuri kuliko hii ya sasa, namuomba mhandisi awe makini haitapendeza skuli ikiwa mpya lakini milango ya zamani ni mizuri zaidi jiangalieni,” alisema.

Alisema dhamira ya serikali ni kuona mambo yaliyoahidiwa katika ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 yanatekelezeka vizuri.

Akizungumzia majengo hayo, Shaka alisema kuna haja ya kuzingatia mambo ya muhimu kuwekwa katika ujenzi wanaoufanya ya dharura ili kuepuka vifo pale majanga yoyote yanapotokea yakiwemo ya moto.

Alisema idadi ya miundombinu ya skuli itaendelea kuongezwa ili kuhakikisha tatizo la msongomano linaondoka.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, walisema wamepokea shilingi milioni 100 kutokana na fedha za mradi wa EP4R Kwa ajili ya ujenzi wa bwalo hilo lakini hazikutosha.