NA MWANTANGA AME

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amekubali kuwa Balozi wa Kuitangaza bidhaa zinazotokan ana zao la  Korosho ya Tanzania, ili liongezeke thamani yake na kuinua uchumi wa Tanzania.

Shaka, aliyasema hayo wakati akizungumza na watendaji wa Kituo cha utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele Wilaya ya Nachingwea, ambao wanasarifu zao Korosho kwa kuzalisha korosho zilizo banguliwa, siagi ya Korosho, Mvinyo wa mabibo, Sharubati ya mabibo, Maziwa na Unga wa Korosho.

Alisema zao la Korosho  hivi sasa linatia tija baada ya serikali kuliimarisha, ili bidhaa zake ziweze kuingia katika soko la hapa nchini na nje ya nchi.

Inafurahisha kuona kituo hicho cha utafiti kimeweza kubaini zao hilo lina uwezo wa kuzalisha vitu mbali mbali, vinavyotokana na Korosho, jambo ambalo litaifanya jamii kuongeza vipato vyao.

“Mimi ninaenda kuwa Balozi wa kuitangaza Korosho, kwani bidhaa hizi ni nzuri nimekula mkate wa korosho ni mtamu sana  sasa inahitajika kujitangaza zaidi kutumia vyombo vya habari” alisema Shaka.

Alisema inapendeza kwa taasisi hiyo kuamua kuzalisha zao hilo kwa kuweka bidhaa mbali mbali ambazo zina uwezo mkubwa wa kukuza uchumi wa nchi na kuongeza upatikanaji wa ajira hapa nchini.

Alisema kitendo cha kituo hicho kuzalisha maziwa, unga wa mikate, mafuta ya Korosho, Alizeti, Ufuta Maziwa ya Korosho na Juisi, pamoja na miche ya mazao mbali mbali ni jambo zuri, kwani bidhaa hizo zitaongeza soko badala ya kutembea Korosho pekee.

Alisema bidhaa hizo zitaifanya jina la Tanzania kupaa zaidi katika uzalishaji wake na kukuza masoko ambayo yataleta tija katika kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa.

Alisema serikali ya Chama cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mwenyekiti wake wa CCM, Samia Suluhu Hassan, katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, imeamua kuitengeneza Bandari ya Mtwara, ikiwa na dhamira kurahisisha usafirishaji wa zao la Korosho ikiwa ni hatua itayowaondolea usumbufu wazalishaji kufika katika masoko kwa wakati.

Alisema wameamua kufanya ziara hiyo ili kujiridhisha matumizi ya Bandari hiyo yanakuwa makubwa badala ya kutumia malori na ndio maana serikali iliamua kutoa fedha kufanyika ujenzi huo.

Hata hivyo, alionya wale ambao wanadhamira ya kuhujumu hatua hiyo kwa kuanzisha mipango ya kutumika kwa bandari hiyo ili waweze kutumia malori yao kusafirisaha Korosho zao.

Hata hivyo Shaka, alimuomba msimamizi wa utafiti katika kituo hicho kuona umuhimu wa kujitangaza kazi zao, ili  watanzania wengi wazifahamu, jambo ambalo litakuza masoko yao na uchumi wa nchi.

Wasimamizi wa Kituo hicho, walisema  hivi sasa wamegundua aina tisa  za mbegu bora za ufuta ambayo itaongeza uzalishaji wake kutoka tani 5.8 kwa mwaka 2018/2019 hadi kufikia tani 36.7 2020/2021.

Vile vile walisema hivi sasa wameanzisha utafiti wa mbegu bora ya michikichi pamoja na kuanzisha kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, ufuta na karanga, ikiwa ni hatua itayoongeza uzalishaji wa bidhaa hizo.