NA HAFSA GOLO
Wananchi wa Shehia za jimbo la Mfenesini wanatarajiwa kupewa elimu ya afya juu ya maradhi ya ili kuweza kukabiliana na maambukizi ya malaria na UVIKO 19.
Mwakilishi wa jimbo hilo,Machano Othman Said aliliambia Zanzibarleo kuwa lengo la kutoa elimu hiyo katika shehia saba jimboni humo ni kuwawezesha wananchi kujua namna bora ya kujikinga na maradhi hayo.
Alisema kuwa katika mpango huo wanakusudia kuwatumia wataalamu wa kinga na tiba kutoka Wizara ya Afya,Ustawi wa Jamii Wazee, Jinsia na Watoto.
Machano alisema, zoezi hilo litahusisha uhamasishaji kuhusu chanjo ya corona, kutumia vyandarua na kuimarishaji wa usafi wa mazingira katika shehia hizo.
Aidha alisema shehia hizo saba zitakazonufaika na mpango huo ni pamoja na shehia ya Kikaongoni, Kihinani, Chuini, Kama, Mfenesini na Bubwisudi.
Sambamba na hilo, Machano alisema viongozi wa jimbo hilo, wameanda mfumo endelevu wa uhamasishaji wananchi wa kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara.
Pia alisema mfumo huo utashajihisha wananchi umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Nae Mwenyekiti wa Vijana jimbo la Mfenesini Bahati Hussein alisema elimu hiyo ni moja ya kati ya utekelezaji wa ahadi za viongozi kwa wananchi wao kuhusu uimarishaji wa afya bora kwa wananchi.
Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili kuhusu utoaji wa elimu ya afya wamesema elimu hiyo itawasaidia kuwapatia taaluma ya kujinginga na maambukizo ya corona.Khalifa Juma Ali alisema,elimu hiyo ni chachu ya maendeleo na ustawi wa afya bora kwa wananchi.