NA ASIA MWALIM

MWENYEKITI wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Khadija Shamte Mzee amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuondoa vikwazo vya Jumuiya na taasisi mbali mbali zilizopo nchini ili kuona wanafanya kazi zao bila vikwazo.

Aliyasema hayo alipokua akifuangua kikao cha wadau wa wa sheria ya NGOs katika kujadili mswaada wa sheria namba 6 mwaka 1995 hafla iliyofanyika ukumbi wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Maisara Zanzibar.

Alisema hatua hiyo imekusudia kutoa nafasi kwa wadau mbali mbali waweze kutoa michango yao juu ya kurekebishwa sheria husika kwa kuondoa maeneo yenye vikwazo kwa kufanafanya kazi zao vizuri.

Alifahamisha kuwa maoni ya wadau hao katika kuchangia sheria za asasi zisizo za serikali kutasidia kupata sheria itakayo kidhi mahitaji yao kulingana na kazi zao kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikwemo suala la uteuzi utakaozingatia suala la jinsia na watu wenye mahitaji maalumu.

Mwenyekiti huyo alisema NGOs zinaisaidia serikali kuondoa matatizo ya jamii kutokana na shughulika mbali mbali wanazozifanya katika jamii ikiwemo uhifadhi wa mazingira, Afya, ulinzi wa kudumisha amani na elimu ya kuepuka vitendo vya udhalilishaji.

Alieleza kuwa kikao hicho kimekusanya NGOs tofauti kwa pamoja ili kila kundi liwasilishe maoni yao kwa maslahi ya wote hivyo wameamua kufika kwao kila mmoja ana uwezo wa kuchangia maoni yake kulingana na kasoro alioina imewabana.

Akiwasilisha muhtasari wa mswaada huo, Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Mussa Kombo alisema maoni ya vikao vilivyopita yamezingatiwa na kuingizwa baadhi ya mambo kwenye rasimu hiyo ili kupata sheria inayogusa maslahi ya wananchi husika.

Alisema jina la sheria ya sasa itaweka asasi zote, pia imezingatia suala la misingi ya asasi hizo ikiwemo uhiari wa wanachama, kwenye suala la kujiunga na kujiondosha, pia utendaji uzingatie misingi ya uwazi, ukweli na usawa kwa maendeleo ya wananchi.

Nae Mrajis wa NGOs Zanzibar, Ahmed Khalid Abdallah alisema Jumuiya Zisizo za Kiserikali, zina mchango mkubwa katika taifa hili kwa kufanya kazi na wananchi kutatua matatizo ya jamii hivyo kuna umakini wa kupitia sheria hiyo ili kuwapa nguvu ya kuwawezesha.