KIGALI, RWANDA

PAUL Rusesabagina,nyota wa filamu iitwayo “Hotel Rwanda”, aliyegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rwanda, amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya ugaidi kufuatia kesi ambayo waungaji mkono wake wanasema ilikuwa ya kimaonyesho iliyochochewa na sababu za kisiasa.

Mahakama kuu ya Rwanda ilimhukumu Rusesabagina kifungo hicho baada ya kumpata na hatia ya kujihusisha na kundi la waasi linalotuhumiwa kuhusika na mashambulio ya umwagaji damu ya utumiaji bunduki, magurunedi na uchomaji moto nchini humo katika miaka ya 2018 na 2019.

Akisoma adhabu aliyopewa mshitakiwa mwishoni mwa kesi hiyo iliyoendeshwa kwa muda wa miezi saba, Jaji Beatrice Mukamurenzi alisema, Rusesabagina aliunda shirika la kigaidi lililoishambulia Rwanda,na akachangia kifedha pia kufadhili harakati za kigaidi.

Waendesha mashitaka waliiomba mahakama itoe hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 67,aliyekuwa mmiliki wa hoteli kwa kuokoa maisha ya watu zaidi ya 1,200 wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 kutokana na hatua alizochukua wakati wa matukio hayo,ambayo ndiyo yaliyotoa ilhamu ya kutengezwa filamu ya Hotel Rwanda.