NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAM

MASHABIKI wa klabu ya soka ya Simba na wasahabiki wa michezo nchini jana walikuwa na wakati mzuri waliposhuhudia shangwe wakati wa kilelel cha ‘Tamasha la Simba Day’, lililofanyika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam jana.

Zilikuwa ni dakika 90 za nyota wa Simba hasa wapya kutambulishwa na kuonesha ubora wao kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo pamoja na wadau wa soka nchini.

Mabingwa hao wa mara nne wa ligi kuu ya Tanzania bara walishuka uwanjani kuikaribisha TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mashabiki wa Simba walifurika kwenye uwanja huo tokea 3:00 za asubuhi huku wengi wakionekana kuwa na hamu ya kuwashuhudia wachezaji wao baada ya kukamilika kwa mchakato wa usajili pamoja na kambi ya kujiandaa na msimu ujao.

Ikicheza bila ya nyota wao wawili kwa mara ya kwanza kwenye tamasha hilo, Clatous Chama na Luis Miquissone, waliouzwa RS Berkane na Al Ahly, walishusha kikosi kilichosheheni nyota kadhaa wa kimataifa.

Baadhi ya nyota hao Pape Sakho, Sadio Kanoute, Peter Banda, Duncan Nyoni, Enock Ibanga, Israel Patrick, Yusuph Mhilu, Kibu Denis, Jeremiah Kisubi, Abdulswamad Kassim na Jimmyson Mwanuke.

Mbali ya burudani za ndani ya uwanja, kulikuwa na burdani za nje ya uwanja zilizotolewa na wasanii mbalimbali ikiwemo bendi kongwe ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta.