NA ABOUD MAHMOUD

ZAIDI ya shilingi milioni 78 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya michoro ya ujenzi wa skuli ya sheria inayotarajiwa kujengwa Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora, Seif Shaaban Mwinyi mara baada ya kumaliza kutia saini mkataba kati ya Wizara na Wakala wa Majengo Zanzibar, huko ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Unguja.

Katibu Mkuu huyo, alisema kuwepo kwa jengo hilo litasaidia kuimarisha masuala ya nchini kwa watakaopata elimu kupitia skuli hiyo.

Alisema kutokana na kazi ya kufanya michoro hiyo imeshaanza na inatarajiwa kumalizika kwa muda siku 28, amewataka wakala hao wa majengo kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa na kutumia umakini wa hali ya juu.

“Kama mlivyosema kazi hii mtaifanya kwa siku 120 na kazi tayari imeshaanza hivyo, kila mkituletea mapema itakua ni faraja zaidi kwetu,”alisema.

Katibu Seif, aliipongeza ZBA kwa kutumia njia mbadala na za urahisi katika kutekeleza kazi zao kwa urahisi na ufanisi wa hali ya juu.

Aidha, Katibu huyo alisisitiza na kuziomba taasisi nyengine  kuitumia taaisi hiyo, ili kuhakikisha majengo ya Serikali yanapata wasimamizi bora na uimara unaostahiki.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), Dk. Kassim Ali Omar, ameishukuru Serikali kwa kuaminiwa na kupewa kazi hiyo ya mchoro wa jengo hilo na  ameahidi kufanya kazi hiyo na kumaliza hatua hiyo ya awali  kwa muda uliowekwa .

“Ahadi yangu kwenu ni kuhakikisha kazi hii mliotupa kwa kutuamini tunaifanya kwa umakini mkubwa na kwa muda uliowekwa,”alisema