NA HAFSA GOLO
SERIKALI imetangaza dhamira yake ya kuwapatia makaazi familia tatu zilizopata athari za mvua masika zilizonyesha mwaka 2020, katika kijiji cha Kidombo Mkwajuni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, ameyasema hayo, Mkwajuni Uyagu, mara baada ya kufanya ziara ya kuwatembelea wananchi walioathirika na mvua za masika za mwaka 2020.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya nane imejiweka karibu na wananchi kwa kuwasikiliza shida zao, kwani ndio walio wachagua na kwaweka madarakani.
“Serikali inaendelea kusimamia kwa vitendo dhamira ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Mzee Abeid Amani Karume katika kuwapatiwa huduma bora wananchi ikiwemo makaazi bora ya kudumu”,alisema.
Aidha, alisema kuwa ni vyema wananchi kujiepusha na kujenga sehemu ambazo zinakaa maji ambayo hupelekea maafa na kusababisha athari mbali mbali kwa wananchi ikiwemo kupoteza mali na kuhatarisha usalama wao pale wanapoingiliwa na maji ya mvua.
Sambamba na hilo, Dk. Khalid alisema serikali inampango wa kujenga mtaro wa maji na kuweka kalvati, ili kuepusha changamoto ya uingiaji wa maji katika makaazi ya watu na waweze kufanya shughuli zao za kijamii bila ya kikwazo.
Akielezea athari zilizo jitikeza katika eneo hilo sheha wa shehia ya Mkwajuni Uyagu, Hussein Haji Kesi, alisema kuwa jumla ya nyumba 28 ziliharibiwa na mvua na kupelekea wananchi wengi kukosa makaazi ya uhakika.