NA LAYLAT KHALFAN
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Khadija Khamis Rajab, amesema serikali ina azma ya kuchukua hatua za kutetea maslahi ya wafanyakazi ,ili kustawisha hali zao kiuchumi.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha nne cha Kamati tendaji ya Shirikisho hilo, kikiwa na lengo la kupitia kazi zote kwa kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu kikao kilichofanyika katika ukumbi wa walemavu jijini Zanzibar.
Alisema Wizara imegundua kuna mambo mengi ambayo yanaendelea kuwakwamisha wafanyakazi katika kupiga hatua mbele, ikiwemo kima cha chini cha mishahara hususan katika mashirika mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuna vilio vingi vya wafanyakazi hususan kwenye chama cha walimu kwa kutojua fedha ya mchango wanayotoa inakwenda maeneo gani, hivyo kuwepo kwa vikao kama hivyo vitasaidia kuwapatia ufumbuzi wanachama hao.
“Vikao vya utendaji ndio roho ya shughuli za utekelezaji wa kazi za kila siku, kwani bila ya vikao hivyo wanachama wenu watakuwa hawawaelewi nakupeleka migogoro ndani ya vyama hivyo”, alisema.
Akizungumzia amani na usalama, Khadija alisema katika nchi sijukumu la serikali pekee bali wananchi nao wanawajibu wa kufanya hivyo ili yale wanayoyahitaji yaweze kufikiwa.
Aliahidi kusimamia sheria ili vikao vinavyofanyika viende sambamba na sera ya vyama hivyo na kuepusha usumbufu unaojitokeza kila mara.
“Mimi kama mtanipa mashirikiano ya dhati basi hizi changamoto zenu ikiwemo mabadiliko ya sheria ambayo imetajwa kuwa ndio chanzo cha matatizo nani ya vyama hivi, hivyo ushirikiano wenu ni muhimu ili kuweza kufikia malengo”, alisema.