NA ASYA HASSAN

KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Edward Sokoine, amesema ipo haja ya kuundwa upya na kuimarisha vikundi kazi vilivyopo kwenye jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa bahari ya hindi (IORA). 

Sokoine alisema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha wadau wa jumuiya hiyo kilichowashirikisha maofisa kutoka taasisi za serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kilichofanyika ktika ukumbi wa ZURA, wilaya ya Mjini Unguja.

Alisema hatua hiyo itasaidia kurahisisha utendaji wa kazi zao pamoja na kulinda maslahi mapana ya taifa hivyo hatua hiyo lazima iende sambamba na malengo ya serikali katika utoaji wa huduma.

Alifahamisha kwamba serikali zote mbili zimejipanga kutumia rasilimali zilizopo katika bahari ya Hindi na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuwavutia na kuwasaidia wananchi wa ndani na hata wa nje kunufaika nazo na kuleta tija kubwa ndani ya taifa.

Sambamba na hayo alifahamisha ni matumaini yake kwamba kikao hicho kitaweza kuendeleza kutathmini endapo kuna wadau wamesahaulika ni vyema kujumuishwa ili kuona kila sekta inakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa masuala ya IORA ili kuleta tija na maslahi mapana ndani ya nchi hizo.

“Licha ya kuwepo kwa vikundi tofauti ndani ya jumuiya hiyo ipo haja ya kuchunguzwa na kutathminiwa ili kuona vinakwenda sambamba katika    kutekeleza mikakati ya uchumi wa buluu ambao unalenga kuimarisha sekta ya uvuvi hususan uvuvi wa bahari kuu,” alisema.

Aidha alifahamisha kwamba serikali zitaendelea kuimarisha sekta ya bahari kwa kuimarisha miradi mbali mbali ili kusaidia kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola, alifahamisha kwamba lengo la kikao hicho ni kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika jumuia ya IORA na kuimarishwa kwa vikundi kazi ili kuona vinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Ofisi ya Mambo ya nje Zanzibar, Balozi, Masoud Balozi alisema mkutano huo ni moja ya kujadili matumizi sahihi ya bahari kuu katika kutekeleza na kusimamia miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo ziliyopo katika uchumi wa buluu.