DAMESKI, SYRIA

WIZARA ya mambo ya nje ya Syria imelaani hatua za Uturuki za kukiuka mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa Syria ina haki ya kujibu chokochoko hizo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetangaza kuwa, nia ya chama tawala nchini Uturuki cha Uadilifu na Ustawi hususan katika kuunga mkono ugaidi na makundi ya kigaidi yaliyotajwa katika orodha ya Baraza la Usalama la UN inazidi kubainika wazi kadri nchi hiyo inavyoendelea kuvamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria.

Wizara ya Mambo ya nje ya Syria ilibainisha kuwa, kumetolewa taarifa za kuingia kinyume cha sheria Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar katika ardhi ya Syria na kufanya vikao mbalimbali na makamanda wa makundi ya waasi huko kaskazini mwa mji wa Halab (Aleppo) ambazo zinathibitsha jinsi ardhi ya Syria inavyovamiwa waziwazi na kupuuzwa maazimio ya Baraza la Usalama.

Wizara hiyo ilisema pia, Ankara inayaunga mkono waziwazi makundi ya kigaidi nchini Syria, kuyafadhili kifedha na kuyapatia silaha.

Vile vile imeashiria wizi wa maliasili za nchi hiyo na kuharibiwa miundo mbinu ya Syria vinavyofanywa na makundi hayo yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na Uturuki na washirika wake.