NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tabia Maulid Mwita, amesema Wizara yao katika utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020/2025, imewataka kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi  wote wakiwemo watu wenye ulemavu.

Waziri Tabia, aliyaeleza hayo alipokuwa akikabidhiwa vifaa vya michezo vya watu wenye ulemavu wa mkono mmoja na mguu mmoja (Amputee) vilivyotolewa na Shirkisho la Kimataifa la Masalaba Mwekundu, huko katika ukumbi wa VIP Amaan mjini hapa.

Alisema katika miongozo ambayo imetoka kwenye ilani hiyo haijasema kama watu wenye ulemavu wasipewe huduma.

Alisema hatua hiyo inaenda sambamba na matakwa ya katiba ya nchi ambayo inawaona na wao ni watu kamili na wana haki sawa na wengine.

Hivyo aliwataka kuona kwamba wizara hiyo ni ya kwao na wanayo haki muda wowote kwenda na kufuata huduma katika Wizara hiyo.

“Tukipata tu utaratibu basi wahakikishe Wizara yetu hii tutakaa pamoja na kuhakikisha tunakaa pamoja na kuyatengeneza yaliyo ya kwenu na kuyaweka sawa”, alisema.