NA ABDI SULEIMAN

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, amesema kufanyika resi za ngalawa na mbio za baskeli Pemba, ni moja ya ishara ya kutangaza utalii wa kisiwa hicho.

Waziri Tabia aliyaeleza hayo wakati alipokua akifungua resi za ngalawa na mbio za baskeli katika kijiji cha Tumbe, ikiwa ni shamrashamra za tamasha la utamaduni wa mzanzibari ambalo hufanyika kila mwaka.

Akizungumza na wanamichezo hao, alisema kufanyika kwa mashindano hayo ni moja ya ishara muhimu, kutangaza utalii ya Pemba kwa kutumia ngoma mbali mbali za asili.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya kuona michezo mingi ya asili imekua ikipoteza uasilia wake, licha ya waanzilishi wake kutoka maeneo ya Tumbe.

Nahodha Kombo Suleiman Zaharan  mwenye ngalawa ya Tetema, aliomba serikali kuhakikisha wanaongeza michezo mengine pamoja na kushajihisha ngalawa nyingi katika mashindano hayo.

Alisema mashindano ya resi za ngalawa sasa yameanza kupotea kutokana na kuwepo boti za kisasa, pamoja na vijana kutokua tayari kurithishwa fani hiyo.

Hata hivyo aliitaka serikali kuandaa mashindano makubwa ya resi za ngalawa yatakayowashirikisha ngalawa kutoka Unguja na Pemba, kama ilivyokua miaka ya nyuma.

Katibu mkuu wizara hiyo  Fatma Hamadi Rajab alisema wizara itaendeleza mila na utamaduni wa Zanzibar.

Naye Adinani Iliyasa Sleimana mshindi wa kwanza katika mbio za baskeli, aliomba wizara kuhakikisha inarudisha mashindano ya mbio hizo, pamoja na kuwatafutia wafadhili.

Mshindi wa kwanza katika resi za ngalawa ilikuwa ngalawa ya Tetema na kupata shilingi 400,000, mshindi wa pili ngalawa Shinogo ilipata shilingi 300,000, mshindi wa tatu ngalawa Zilipendwa ilipata 200,000 na washiriki wakipatiwa 100,000.

Kwa upande wa mbio za baskeli mshindi wa kwanza alikuwa ni Adinani Ilyasa aliyepatiwa shilingi 150,000 mshindi wa pili 100,000 na wa tatu ni 80,000.