NA LAYLAT KHALFAN

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar  ina mpango wa muda mrefu wa kuongeza maeneo ya viwanja vikiwemo viwanja vya wilaya na Taifa.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tabia Maulid Mwita, huko Baraza la Wawakilishi wakati wa akijibu suali la mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Yahya Rashid Abdulla,  alietaka kujua serikali ina mpango gani wa kuongeza maeneo ya viwanja baada ya viwanja vingi kuvamiwa.

Aliyataja baadhi ya maeneo ya zaidi ambayo yapo katika mpango huo ni Tunguu, Fumba, Jendele na Hanyegwa Mchana.

Aidha alisema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi watatenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo wakati wa kuandaa mipango miji na vijiji.

“Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa serikali inafahamu kuwa viwanja vingi vimevamiwa na baadhi ya maeneo wananchi wanakosa sehemu za kucheza”, alisema.

Hata hivyo alisema kwamba sera ya michezo ya mwaka 2018 na Ilani ya CCM ya 2020 – 2025 inaelekeza kulinda na kuendeleza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo.

Alifahamisha kwamba suluhisho kuu la  tatizo hilo ni kuyapima na kuyaendeleza ili wananchi waweze kucheza, kuongeza maeneo ya viwanja vikiwemo viwanja vya wilaya.