HAFSA GOLO NA MUZNAT HAJI (SCCM)

WAZIRI wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Tabia Maulid  Mwita amesema wizara hiyo, iliahidi kutoa ushirikiano katika suala zima la mazoezi kwa vijana na sio kudhamini mazoezi.

Alitoa kauli hiyo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi  wakati akijibu suali lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Pandani Omar Fakih Hamad, alipotaka kujua kuwa udhamini huu ni kwa ajili ya mazoezi ya vijana wa Chama cha Mapinduzi  (UVCCM) pekee yao au kuna fursa kwa vijana wa vyama vyengine kudhaminiwa.

Alisema chombo cha kudhamini na kuratibu masuala yote ya vijana ni Idara ya Vijana pamoja na Baraza la Vijana.Tabia alisema,wizara hiyo itaendelea kuwashajihisha vijana wote kushiriki katika kufanya mazoezi kwani mazoezi hujenga afya ,udugu na urafiki.

Akitilia mkazo suala hilo alisema,hakuna program  yoyote katika bajeti ya 2021/2022, ambayo imepangwa kwa ajili ya kutoa udhamini wa mazoezi, bali kupitia sera ya michezo ya mwaka 2018 inaitaka wizara kuwasaidia wanamichezo kuibua vipaji vyao ikiwemo kushajihisha mazoezi.

“Serikali inafanya juhudi za makusudi za kudhamini maendeleo mbali mbali ya vijana wote, bila ya mgongano wa maslahi kupitia program mbali mbali za miradi ya vijana ambazo zinaendelea kuwanufaisha vijana wote wa Zanzibar bila ya kujali itikadi ya chama ”,alisema.