KABUL, AFGHANISTAN
TAARIFA kutoka nchini Afghanistan zimesema watawala wapya wa taifa hilo vuguvugu la Taliban huenda wakatangaza serikali yao huku dunia ikusubiri kwa shauku kuona iwapo utawala mpya utatimiza ahadi zao kwa Afghanistan.
Tangazo hilo, ambalo vyanzo viwili vya Taliban vililiambia shirika la habari la AFP kwamba linaweza kutolewa baada ya jana sala ya Ijumaa, linafanyika siku kadhaa baada ya Marekani kuondoa kikamilifu wanajeshi na kuhitimisha vita vilivyodumu kwa miaka 20.
Mataifa ya Magharibi yalikumbatia mkakati wa kusubiri na kuona kuhusu ushirikiano wao na kundi la Taliban kuendelea mbele, lakini kumekuwepo na ishara za kuregeza msimamo baada ya makampuni ya uhamishaji fedha ya Western Union na MoneyGram kutangaza kuanza tena kutoa huduma kuelekea taifa hilo.
Qatar ilisema ilikuwa inafanya kazi kuufungua tena ubalozi wake mjini Kabul, huku China ikiripotiwa kuahidi kuacha wazi ubalozi wake na kuimarisha zaidi uhusiano na msaada wa kibinadamu.
Uvumi ulienea kuhusu muundo wa serikali mpya ya Afghanistan, ingawa ofisa mmoja mwandamizi alisema wiki hii kwamba wanawake wana uwezekano mdogo wa kujumlishwa.