HATIMAYE maal-watan wa Taliban wametangaza serikali mpya ya mpito itakayoliongoza taifa la Afghanistan, kufuatia kuchukua madaraka kwa mtutu wa bunduki kwa kuvishinda vikosi dhaifu vya iliyokuwa serikali ya nchi hiyo.

Mnamo Agosti 15 mwaka 2021, baada vikosi vya Taliban kudhibiti miji na wilaya kadhaa nchini humo hatimaye walifanikiwa kuukamata mji mkuu wa nchi hiyo na kuikamata ikulu ya rais Ashraf Ghani ambaye alilazimika kuingia mafichoni ughaibuni.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kundi hilo, Mullah Mohammad Hassan Akhund ameteuliwa kuwa mkuu mpya atakae iongoza serikali ya Afghanistan.

Msemaji wa kundi hilo Zabiullah Mujahid aliwaambia waandishi wa habari mjini Kabul kwamba Mullah Mohammad Hassan Akhund, alikuwa waziri wa ngazi ya juu katika utawala wa zamani wa Taliban katika miaka ya 1990.

Mullah Mohammad Hassan Akhund

Kwa mujibu wa utawala wa sasa wa Taliban, Mullah Mohammad Hassan Akhund atachukua dhamana ya kuongoza shuhguli za serikali kama waziri mkuu.

Kiongozi huyo mpya wa Afghanistan kutoka kundi la Taliban, Hassan Akhund ni miongoni mwa watu ambao wanakabiliwa na vikwazo na Umoja wa Mataifa.

Kundi la Taliban limeahidi kuunda serikali itakayojumuisha kila jamii nchini humo, lakini nyadhifa zote za juu zimekabidhiwa viongozi wakuu wa vuguvugu hilo na mtandao wa Haqqani ambao ni tawi la Taliban.

Katika orodha ya viongozi wa serikali waliotangazwa hakuna mwanamke hata mmoja. “Tutajaribu kujumuisha watu kutoka maeneo mengine ya nchi, hii bado ni serikali ya mpito”, alisema Zabiullah Mujahid.

Msemaji huyo kabla ya kuundwa kwa serikali hiyo alisema kuwa mujibu wa hukumu za kur-ani na sharia za dini wanawake hawawezi kuwa mawaziri, lakini hakuna kizuizi chochote kufanya kazi katika sekta za tiba na elimu.

Muda mfupi tu baada ya majina ya maofisa wa serikali mpya kutangazwa, Hibatullah Akhundzada ambaye ni kiongozi mkuu wa Taliban ambaye hajawahi kuonekana hadharani, alitoa taarifa iliyoitaka serikali mpya kufanya bidii katika kuzingatia na kulinda sheria za kiislamu na kutii Sharia.

Mullah Yaqoob ambaye ni mwanawe mwanzilishi wa kundi hilo ambaye pia alikuwa kiongozi mkuu marehemu Mullah Omar alitangazwa kuwa waziri wa ulinzi, huku nafasi ya wizara ya mambo ya ndani ikikabidhiwa kwake Sirajuddin Haqqani ambaye ni kiongozi wa mtandao wa Haqqani.

Muasisi mwenza wa Taliban, Abdul Ghani Baradar ambaye alisimamia utiaji saini wa makubaliano ya vikosi vya Marekani kujiondoa Afghanistan atakuwa naibu wa waziri mkuu.

“Si ajabu kwa njia yoyote kwamba serikali iliyotangazwa na Taliban haijawajumuisha Waafghani wote. Kundi hilo halikuwahi kudokeza kuwa baraza lake la mawaziri litajumuisha wasiokuwa watu wao,” amesema Michael Kugelman ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kusini mwa bara Asia katika taasisi ya wasomi ya Woodrow Wilson.

Lakini wakati Taliban linapojibadilisha kutoka kundi la kivita na kuwa kundi la kiutawala, maofisa wake wa usalama wanakabiliwa na ongezeko la maandamano yanayopinga utawala huo.

Je serikali ya mpya ya Afghanistan itaungwa mkono duniani?  Kwa mujibu wa msemaji wa Taliban Zabiullah Mujahid amesema kuwa nchi za China, Qatar na Uturuki zimekuwa washirika wakuu wanaoiunga mkono serikali hiyo.

Mujahid alisema nchi za China, Uturuki na Qatar ni washirika wakuu wa kundi hilo na wameonesha utayari wao wa kusaidia ujenzi wa mpya wa taifa hilo lililovurugwa kwa vita vilivyochukua takriban miaka 20.

Mujahid aliliambia gazeti la Repubblica linalochapishwa nchini Italia akisema kuwa “washirika wetu wakuu kwa ajili ya ukarabati na kuijenga upya Afghanistan ni China, Qatar na Uturuki na tunafanya jitihada kupitia China ili tuweze kuingia kwenye masoko ya dunia”, alisema.

Katika maelezo yake, Mujahid aliongeza kueleza kuwa katika mataifa hayo China ndiye mshirika muhimu zaidi wa kibiashara na kiuchumi wa Taliban na kwamba taifa hilo limeonesha utayari wa kuwekeza miradi ya kiuchumi nchini humo.

Alibainisha kuwa mtazamo wa kundi hilo, mpango wa kuanzisha ukanda na barabara kuu ya China una umuhimu mkubwa na kueleza kuwa Afghanistan ina utajiri mkubwa wa madini ya shaba na China inaweza kuifufua migodi ya madini hayo kwa kuipatia nchi hiyo teknolojia ya kisasa ya uchimbaji madini.

Alipoulizwa kuhusu Urusi, Mujahid alisema nchi hiyo ni nchi muhimu na kwamba Taliban ina uhusiano mzuri na nchi hiyo kama mshirika muhimu.

Aliongeza kuwa uhusiano wa Taliban na Urusi ni wa kisiasa na kiuchumi na kwamba Moscow inafanya juhudi za upatanishi wa kuleta suluhu kimataifa kwa manufaa ya kundi hilo.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umeainisha masharti yanayoelezea kiwango cha namna itakavyojihusisha na Taliban ambao ni watawala wapya wa Afghanistan ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binaadamu.

Masharti hayo pia ni kuheshimu utawala wa sheria. Tayari umoja huo umewaondoa mabalozi wake nchini humo tangu wanamgambo hao walipochukua udhibiti mwezi uliopita.

Licha ya masharti hayo yaliyotagazwa na Umoja wa Ulaya umoja huo umesema uko tayari kushirikiana na Taliban, kwa kuwa sasa ndio watawala.

Kufuatia mikutano na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ulaya huko Slovenia, mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya Josep Borrell alisema kwamba ili kupima nia njema ya Taliban, Umoja huo unatakiwa kuwa na misingi kadhaa, ambayo ni pamoja na kujihakikishia kuwa Afghanistan haitakuwa kituo cha kusambaza ugaidi kwenye mataifa mengine.

“Mawaziri wamesisitiza sana kwamba tuendelee kuwasaidia watu wa Afghanistan. Ili kuwasaidia tunatakiwa kushirikiana na serikali mpya, lakini haimaanishi kwamba tunaitambua. Na hilo ni kupima tabia tunahitaji misingi.

Tutapima tabia ili tushirikiane nao kulingana na serikali inavyowajibika kwa Waafghanistan na sio kuwa kama kituo cha kusambaza ugaidi kwenye mataifa mengine,” alisema Borrell.

Suala jingine kulingana na Borrell ni kuwa na msingi wa uanzishwaji wa serikali jumuishi na ya mpito kupitia makubaliano miongoni mwa makundi ya kisiasa nchini Afghanistan, lakini pia kuruhusu misaada ya kibinaadamu na kuheshimu mchakato na masharti ya kufikishwa misaada hiyo.

Masharti mengine yanahusiana na namna Taliban itakavyowajibika katika hatua ya kuwaondoa raia wa kigeni waliosalia nchini humo na Waafghanistan wanaotaka kuondoka.

Katika hatua nyingine katibu mkuu wa jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema muungano huo utaangazia namna ya kuwaondoa Waafghanistan wengi zaidi wanaokabiliwa na kitisho na kuendeleza mahusiano na Taliban, lakini akisema, watawala hao wapya wanatakiwa kudhihirisha kwamba wanastahili kusaidiwa na kutambuliwa.

Alionya dhidi ya hisia kwamba wataitambua kirahisi serikali ya Taliban, wiki mbili baada ya wanamgambo hao kuidhibiti Kabul na kusema ni mapema mno kumtambua mwanzilishi mwenza wa Taliban, Mullah Baradar kama kiongozi mteule wa serikali mpya.

Uturuki, ambaye ni wanachama wa NATO, ambayo imekuwa ikiusimamia uwanja wa ndege wa Kabul kwa miaka sita, imeahidi kuendelea kuuendesha, kwa kuwa sasa Wamarekani na majeshi mengine ya NATO wameondoka.