NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), kinaviomba vyombo vya ulinzi kuhakikisha vinafanya uchunguzi na kuwatia mbaroni wahusika wa vitendo vya mauaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Chama hicho, Dk. Mzuri Issa, imeeleza kuwa matukio ya mauaji na upigaji wa watoto na wanawake yamekithiri katika siku za hivi karibuni.

Katika taarifa hiyo, Dk. Mzuri alisema vyombo vya ulinzi vina jukumu la kuhakikisha vinafanya uchunguzi wa kina na kuwabaini wahusika wa matukio hayo na hatimaye kuwafikisha mahakamani.

Taarifa hiyo ya TAMWA imekuja wakati hivi karibuni msichana wa miaka 23 Sumaiya Mohammed Said mkaazi wa Jambiani Kikadini mkoa wa Kusini Unguja anadaiwa kuuawa kwa kupigwa mapanga na   Imani Abdallah Abdallah umaarufu Kichele (38).

Tukio jengine la ukatili dhidi ya wanawake limetokea Fuoni nyumba moja mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo Raya Khamis Mgeni (45), anadaiwa kushambuliwa kwa mapanga yeye na mtoto wake aliye chini ya umri wa mwaka mmoja.

Katika tukio hilo la Fuoni, shambulizi hilo limesababisha kifo cha mtoto huyo asiye na hatia, huku Raya akijeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Mnazi mmoja tangu Agosti 30 mwaka huu.

“TAMWA inaviomba sana vyombo vya ulinzi kukomesha vitendo hivi kwa kuwatafuta wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili wapewe adhabu inayowastahiki”, ilieleza taarifa ya Dk. Mzuri.

Aidha alifafanua kuwa kuvamiwa wanawake na watoto na kupigwa ni uvunjifu wa haki ya msingi ya kuishi kwa amani na pia inawatia hofu katika kuendeleza shughuli za kimaendeleo.

Kwa mujibu wa rikodi za TAMWA ZNZ, inaonesha kuwa tangu mwaka 2016, matukio 19 ya mauaji ya wanawake na watoto yameripotiwa, ambapo wanawake ni 15 na watoto wanne.

Katika matukio hayo machache tu ndiyo yaliyofikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar yakiwemo ya Wasila Mussa (21) na Hajra Abdallah Abdallah (21).