NA MATHIAS CANAL, DODOMA

WAZIRI wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema mahindi yayanyofikia tani 90,000 yatanunuliwa na wakala wa taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA), ambapo ununuzi wa zao hilo utaanza kwenye mikoa saba.

Prof. Mkenda alieleza hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa baada ya rais Samia Suluhu Hassan kutoa shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuiwezesha NFRA kununua mahindi kwa wakulima wadogo.

Waziri huyo alitaja mikoa ambayo NFRA itaanza kununua mahindi kuwa ni Ruvuma, Rukwa, Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Iringa huku CPB ikinunua mikoa sita ambayo ni Rukwa, Katavi, Njombe, Songwe, Dodoma na Manyara.

Alifahamisha kuwa mahindi hayo yatanunuliwa kwa bei ya shilingi 500 kwa kilogramu huku bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko (CPB) ikinunua mikoa sita kwa bei ya soko.

Alibainisha kuwa mwaka huu zimezalishwa tani milioni sita za mahindi huku ziada ikiwa mara mbili ya uzalishaji uliofanyika kwa mwama uliopita ambapo nchi za Zimbabwe, Zambia zikitajwa kuzalisha kwa wingi nafaka hiyo.

Alisema mahindi hayo yatanunuliwa kupitia vyama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) au vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa na kwa wakulima wadogo kwa magunia yasiyozidi 300 au tani 30 kwa kuwa wanataka rekodi ya kila mkulima aliyelima mahindi yanunuliwe na fedha zilizotolewa na serikali zitumike kama ilivyokusudiwa.

Alisema baada ya zoezi hilo kufanyika wizara itafanya ufuatiliaji kwa viongozi wa mikoa ili kupata taarifa na namna mgawanyo wa ununuzi ulivyofanyika kwenye mikoa tajwa.

“Tutakagua hivyo wananchi au wakulima mkiona dalili za ukiukwaji wa ununuzi wa mahindi toeni taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo kwenye maeneo yenu,” amebainisha.

Ofisa Mtendaji Mkuu NFRA, Milton Lupa alisema wanakwenda kununua nafaka hiyo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwenye mikoa ya Songea, Ruvuma, Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa kupitia AMCOS na wakulima waliosajiliwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu CPB, Dk. Anselim Moshi alisema watanunua mahindi hayo kama walivyoelekezwa na wizara na kwamba wameshaanza kutafuta masoko nje ya nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Sudani Kusini, Comoro, Burundi na Rwanda.

“Tumetafuta fedha kwa kukopa kwenye benki tutanunua nafaka hiyo kwa wingi na kusafirisha nje ya nchi ambapo ndio tumetafuta masoko kwa ajili ya kuuza”, alisema.