WACHEZAJI timu ya taifa vijana ya soka wanawake   Afghanistan wamevuka mpaka kuingia Pakistan.

Wasichana hao walikuwa wametumia mwezi uliopita wakiwa wamejificha kwa hofu ya kukandamizwa kwa haki za wanawake na kundi la Taliban lililoingia madarakani.

Timu ya soka ya taifa ya watu wazima iliondoka Kabul mwezi uliopita lakini timu ya vijana inasemekana waliachwa, wakiwa hawajui la kufanya kwasababu ya hawakuwa na pasipoti na nyaraka nyingine muhimu.

Wachezaji 32 na familia zao walipata visa baada ya ushawishi wa chama cha serikali cha “Football for Peace”.

Maafisa walisema kundi hilo, jumla ya watu 115, watasafiri kutoka Peshawar kwenda mji wa mashariki wa Lahore, ambapo watapewa makazi katika makao makuu ya Shirikisho la Soka la Pakistani.

Gazeti la Independent hivi karibuni liliweka wazi kwamba wachezaji hao walikuwa wamemwandikia Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, kuomba ruhusa ya kuingia nchini humo kwa haraka.

Barua hiyo ilidai kwamba wasichana hao walikuwa katika “hatari ya tishio kubwa” kutoka kwa Taliban.

Baada ya kuanguka utawala wa serikali ya Afghanistan, wachezaji wa Kabul walionywa na nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Khalida Popal, kufuta picha zao zote wakicheza zilizopo kwenye mitandao ya kijamii na kuchoma vifaa vyao vyote ikiwemo sare ili kuepuka ukandamizaji unaoweza kutokea kutoka kwa serikali mpya.

Wiki iliyopita naibu wa tume ya kitamaduni ya Taliban, Ahmadullah Wasiq, alitonyesha shaka juu ya mustakabali wa michezo ya wanawake nchini humo, wakati alisema haionekani kuwa “inafaa wala yenye ulazima,” akijibu swali juu ya hatima ya timu ya wanawake ya kriketi.

“Katika mchezo wa kriketi, wanaweza kukabiliwa na hali ambayo uso na mwili wao hautafunikwa. Uislamu hauruhusu wanawake kuonekana kwa namna hiyo”, Wasiq alisema.