NA ABOUD MAHMOUD
ZANZIBAR ni nchi maarufu duniani iliyofanikiwa kuutangaza vyema utamaduni wake katika mataifa mbali mbali pamoja na kurithisha vizazi vyake.

Utamaduni huo umevuka katika nchi mbali na wageni kutoka nchi za nje huja kuangalia na wengine kujifunza kutokana na uzuri wake.

Hili ni jambo jema kwani limesaidia Zanzibar kujulikana katika kila kona ya dunia na kuonesha kwamba nchi hii, ipo makini katika kulinda na kutangaza vyema utamaduni wake.

Kupitia haya katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia kufifia kwa urithishwaji wa utamaduni huo.

Katika kuliona hilo ngoma mbali mbali za utamaduni ambazo zilikua alama tosha ndani ya visiwa vyetu zimepotea na hata vizazi vya sasa ukiwauliza hawazijui.

Miongoni mwa ngoma hizo ni pamoja na tukulanga, bomu,mwanandege na nyengine nyingi, ambazo mtoto aliezaliwa kuanzia mwaka 2000 si rahisi kuzijua.Lakini mbali na ngoma za utamaduni hata ile michezo ya kitoto ambayo watoto wengi, walikua wanacheza imekufa na haijulikani wala haisikilikani katika masikio ya wengi.

Michezo hiyo ni pamoja na mfundo, ukuti,maji ya mdimu,kinyuri nyurika,kula mbakishie baba na mengine mingi, ambayo haisikilikani na watoto wa sasa hivi hawaijui na akili zao zote wamezielekeza katika muziki wa kizazi kipya.

Lakini mbali na hayo katika miaka ya zamani kulikua na utamaduni wa watoto wakati wa usiku kutulia nyumbani na kutolewa hadithi zile zinazojulikana kwa umaarufu wa ‘paukwa pakawa’ ambazo na hizo zote hivi sasa zimepotea.

Kwa kweli hili jambo linasikitisha kwani ule urithi tunaoutaka kuwarithisha vizazi vyetu, haupo na hii inaweza kusababisha Zanzibar ikakosa kujulikana utamaduni wake ni upi.
Katika kipindi cha hivi karibuni kwenye tamasha la Kizimkazi kulipigwa ngoma za asili zinazojulikana kwa jina ls ‘Shoo Moo’ na Moto moto ambazo asili yake ni kutoka katika kijiji cha Mtende na Kizimkazi.

Ngoma hizi ambazo zilionekana kufurahiwa na wengi waliofika kwenye tamasha hilo, wakiwemo wageni na hata wenyeji ambao hawajawahi kuona wala kuzisikii ngoma hizo.
Kwa kweli ngoma hizo ziliibua hisia za wengine na kuonesha kwamba Zanzibar ina utamaduni mkubwa wa ngoma za asilia, ambao unahitaji kuenziwa na kurithishwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kutokana na hilo ni wajibu wetu sote na sio kuiachia jukumu serikali na taasisi zake katika kuhakikisha tunalinda, tunatunza, tunaenzi pamoja na kurithisha utamaduni wetu.
Imani yangu kubwa endapo tutashikamana na kuhakikisha ngoma na michezo ya watoto itaendelezwa katika nchi yetu, maadili yatakawepo kama yalivyokuwa miaka ya nyuma, lakini kwa upande wa ngoma za asili tunaitangaza vyema nchi yetu katika mataifa mbali mbali duniani.

Ni lazima tuige mfano wa nchi za wenzetu kama vile India, Nigeria, na hata falme za kiarabu, ambazo nao wamekua mstari wa mbele kurithisha tamaduni zao kwa vizazi vyao.

Kutokana na hilo na burudani iliyotolewa katika tamasha la Kizimkazi mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na kufurahiwa na wengi,wakati umefika kila mmoja wetu kuhakikisha ngoma hizo na nyengine kuzirudisha ili kurithisha watoto wetu pamoja na kujitangaza kitaifa na kimataifa.