NA KHAMISUU ABDALLAH
TANZANIA bara na Zanzibar ni nchi zenye udugu wa damu baada ya Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalim Julius Kambarage Nyerere pale waliposaini mkataba wa makubaliano wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Hadi tarehe hiyo kulikuwa na mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba huo na kuanzishwa dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar mkataba ambao ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi April 26 mwaka 1964.
Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lilibadilishwa baadaye, Oktoba 28 mwaka 1964, na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile undugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP.
Katika kuona muungano huo unaendelea kuimarika zaidi, viongozi mbalimbali wa serikali wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi waliopita na wasasa wamekuwa wakiendeleza juhudi za kuimarisha muungano huo kwa kutatua kero ambazo zimekuwa hasa kwa Zanzibar.
Hatua hiyo ni pamoja na hoja 11 kuhusu kero za Muungano zimepatiwa ufumbuzi katika kikao cha pamoja kati ya mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chenye lengo la kutatua kero za Muungano.
Hoja hizo 11 zimetatuliwa huku hoja tisa zikiwa zimetengenezewa hati za makubaliano ya pande mbili hizo na hoja mbili hazikuwa na hati kwa kuwa zinaweza kutekelezeka.
Hoja ambazo zimetengenezewa hati ni pamoja na Bahari kuu, Uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar, ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano, Mgawanyo wa misaada inayotoka nje.
Hoja nyengine ni mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ukarabati wa hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, Mkataba wa mkopo wa barabara ya Chakechake hadi Wete Pemba, Mkataba wa mkopo wa ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, Usimamizi wa ukokotoaji na usimamizi wa huduma za simu na mapato yanayokusanywa na uhamiaji kwa upande wa Zanzibar
Kauli ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Philip Mpango ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa kamati hiyo aliwafahamisha watanzania kuwa makubaliano yaliotiwa saini yatakuwa na faida kwa pande zote mbili za Muungano.
Ni jambo la kupongezwa kuona viongozi wetu wa pande zote mbili za Muungano walikaa kwa siku mbili visiwani Zanzibar kuzijadili kero 18 kati ya kero 25 zilizoorodheshwa tangu mwaka 2006 ambapo tayari kero saba zikiwa zimetatuliwa.
Lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha wananchi wa Zanzibar na Tanzania bara wanaendelea kufurahia muungano wao wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Jemedari Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julias Kambarage Nyerere wakati wa uhai wao.
Tunaamini kwamba kuzifanyia kazi changamoto za muungano na kuweza kuzitatua ni kuendelea kudumisha Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar uliokuwa imara miaka yote ikiwemo mahusiano yao na Muungano wao utaendelea kuzidi kuimairka milele na milele.
Ni jukumu la watanzania kuendelea kuimarisha Muungano wao ambao umekuwa na mafanikio makubwa kwa pande zote mbili.