Kuna umuhimu wa kuchanja mbwa, paka

NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)

KILA ifikapo 28 September ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya kichaa cha mbwa (rabies), ambapo hafla hiyo iliadhimishwa siku moja iliyopita.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Jikinge na ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa kuwapa chanjo mbwa na paka kila mwaka”. Kila mwaka kichaa cha mbwa kinakadiriwa kukatili maisha ya takribani watu 60,000 wengi wakiwa vijijini barani Asia na Afrika na tishio linaongezeka.

Lengo la siku ya kichaa cha mbwa duniani ni kuelimisha kuhusu ugonjwa huo na kuchukua hatua za kuutokomeza ifikapo 2030.

Kichaa cha mbwa ni ugonjwa wa kuambukiza unaoathiri mfumo wa kati wa fahamu yaani ubongo na ugwe mgongo na kupelekea kupooza, kupoteza fahamu au kifo.

Ugonjwa huu ni hatari na husabishwa na virusi viitwavyo kitaalam kitaalam kama rabies virus. Vijidudu hivi vinapatikana katika mate au damu ya binadamu na wanyama wengine kama mbwa, mbweha, paka, popo nakadhalika.

Ugonjwa huu husambaa na kuleta madhara zaidi kwa watoto ndani ya muda mfupi chini ya siku 10. Hii hutokana na kinga yao kutokomaa, vilevile watoto huwa karibu sana na wanyama wafugwao na hivyo kupelekea kuumwa au kugusa mate yao.

Tiba yake mpaka sasa haijapatikana kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya virusi, lakini kumekuwepo chanjo ambayo hutolewa kabla au baada ya kuambukizwa ili kuzuia kusambaa na kuleta madhara mwilini. Pamoja na chanjo kama dalili zikiwa zimeshajitokeza kupona huwa sio rahisi.

Kwa takribani miaka 30 iliyopita ni watu 7 tu walipona baada ya chanjo wakiwa na dalili. Kuna mikakati iliyopo ya Umoja wa Kimataifa kuutokomeza ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030.

Kutokana na hali ya kiuchumi nchi zinazoathirika zaidi ni za Africa, hii ndio sababu kubwa ikiwemo Tanzania na Zanzibar kwa jumla kushindwa kutokomeza kichaa cha mbwa ambapo inakadiriwa gharama ya chanjo yake kufikia shilingi 150,000.

KICHAA CHA MBWA JINSI KINAVYOENEA KWA BINADAMU

Kuumwa au kukwaruzwa na mnyama mwenye virusi hivi, ambavyo hupenyeza katika ngozi na kuingia mwilini. Madhara huonekana haraka zaidi kama majeraha yapo karibu na kichwa.

Kugusana na mate ya wanyama na baadae kupitia mdomoni huweza kuingia mwilini, Kwa njia ya hewa kutoka kwa popo na inaweza kuambukizwa kwa kugusa damu ya mnyama mwenye maambukizi ya virusi hivi.

Tofauti na mbwa ambaye amezoeleka kuambukiza ugonjwa huu, pia wanyama kama paka, mbweha, mbwa mwitu na popo wanahusishwa kwenye kuambukiza ugonjwa huu.

DALILI ZA KICHAA CHA MBWA KWA BINADAMU

Mganga Mkuu wa magonjwa ya mifugo Zanzibar, Dk. Talib Saleh Suleiman alizitaja dalili kubwa wanazopata binadamu pindipo wanapopata maambukizi ya kichaa cha mbwa, ugonjwa huanza kuonekana baada ya mwezi hadi miezi mitatu baada ya kung’atwa na mnyama mwenye maambukizi, lakini pia tafiti zinaonyesha kuwahi hadi wiki tatu baada ya kuambukizwa hadi miaka saba.

DALILI HIZI NI KAMA

Homa na kuhisi uchovu mwa mwili, kichwa kuuma na kuchanganyikiwa, kubadilika tabia kuwa mkali kupita kiasi, kukasirika au kuogopa sana, hofu ya maji ‘hydrophobia’, kukosa uwezo wa kutawala mwendo wa viungo vya mwili, kupoteza fahamu.

Dk. Talib aliendelea kwa kusema kwamba mara dalili hizi zinapoonekana maana yake ugonjwa umeshaanza kuharibu ubongo na neva na uwezekano wa mgonjwa kupona kunakuwa ni nadra sana na hivyo basi kifo huweza kutokea.

Aliwashauri wasipuze wito wa kuwapeleka wanyama hao kupata chanjo kwani wanyama hawana dhamana na ugonjwa huu upo hapa visiwani japo wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu sana katika kuutokomesha kabisa.

MATIBABU NA KINGA YA KICHAA CHA MBWA

Tiba ya chanjo kujikinga na maambukizi ya virusi hivi ikitolewa mapema au mara moja baada ya kuambukizwa, lakini tiba inahitaji kutekelezwa kabla virusi havijafikia ubongo, kwa hiyo ni muhimu kupata matibabu katika muda wa saa za kwanza baada ya kung’atwa.

Pia ni kutoa chanjo kwa mbwa wote ili kuwakinga na virusi hivi. Ni muhimu wanyama wa kaya wapewe chanjo dhidi ya ugonjwa huu ili kulinda mbwa kutopata maambukizi ya virusi hivi.

Kuosha mahali palipo umwa au penye mchukubo kwa dakika 15 kwa maji na sabuni au povidoni/iodine, vinaweza kuua virusi pia na kuwa na ufanisi fulani katika kuzuia maambukizi ya kichaa cha mbwa.

Hata hivyo ugonjwa huu unaosambazwa na virusi, unazuilika kwa watu kupewa chanjo ambayo imekuwepo kwa zaidi ya karne. Hivi sasa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wanatoa wito wa kutafakari upya jinsi ya kuzilinda jamii kutopata maradhi hayo.